Watu wanne waliojeruhiwa Brussels wafariki

Polisi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Polisi wameendelea kuwasaka washukiwa Ubelgiji

Watu wanne waliojeruhiwa wakati wa mashambulio ya Brussels wiki iliyopita wamefariki na kufikisha idadi ya waliofariki hadi 35, maafisa nchini humo wamesema.

Hayo yamejiri huku waendesha mashtaka nchini Ubelgiji wakisema watu watatu wameshtakiwa kwa tuhuma za kuwa wanachama wa kundi la kigaidi.

Uchunguzi bado unaendelea kuhusu mashambulio hayo yaliyotekelezwa Jumanne.

Washukiwa hao watatu, Yassine A, Mohamed B na Aboubaker O, walikamatwa wakati wa msako wa maafisa wa usalama Brussels na Antwerp.

Serikali ya Ubelgiji imesema bado ni mapema kujua iwapo uwanja wa ndege wa Zaventem, ulioshambuliwa Jumanne, utafunguliwa tena.

Maafisa wa serikali wamesema wafanyakazi 800 watafanyia majaribio kituo cha muda cha kuhudumia wateja ambacho kimejengwa siku ya Jumanne.

Kwingineko, polisi wa Uholanzi walitangaza Jumapili jioni kwamba walikuwa wamemzuiliwa mwanamume raia wa Ufaransa mjini Rotterdam kufuatia ombi la Ufaransa.

Mwanamume huyo wa umri wa miaka 32 alikamatwa akishukiwa kupanga shambulio Ufaransa na atapelekwa Ufaransa.

Mfaransa huyo anadaiwa kuwa na uhusiano na Reda Kriket, aliyekamatwa Paris mnamo Alhamisi na ambaye maafisa walisema alikuwa katika hatua za mwisho mwisho za kupanga shambulio la kigaidi.