Madaktari walalamikia kushambuliwa na raia Tanzania

Haonga
Image caption Dkt Haonga amesema utaratibu wa kisheria unafaa kufuatwa dhidi ya madaktari wanaokosea

Chama cha madaktari nchini Tanzania kimelalamikia ongezeko la visa vya madaktari kushambuliwa na wananchi nchini Tanzania.

Mwenyekiti wa chama hicho Dkt Billy Haonga amesema vitendo vya madaktari kushambuliwa havikubaliki kamwe.

Alikuwa akihutubia wanahabari baada ya Dkt Dickson Sahini wa hospitali ya rufaa ya Ligula mkoani Mtwara kupigwa na kuvuliwa nguo na watu wanaodaiwa kuwa ndugu wa mgonjwa.

Majuzi, nyumba ya daktari mkoani Katavi ilizingirwa na ndugu wa mgonjwa baada ya jamaa wao kufariki kutokana na ukosefu wa dawa.

“Hata kama daktari amekosea, siyo haki yako kumpiga. Huna haki,” amesema Dkt Haonga.

“Kama daktari huyo alikosea, kitu ambacho kinahatarisha maisha ya mgonjwa, lipo baraza la matabibu. Ashtakiwe huko.”

Mkuu wa mkoa wa Mtwara Henry Mwaibambe amesema watu wawili wanaotuhumiwa kumpiga daktari hospitali ya mkoa wamekamatwa usiku wa kuamkia leo wakitoroka nchi.

Watatu bao wanasakwa na polisi.