Samsung yazindua huduma ya malipo China

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Huduma ya malipo ya simu yazinduliwa na Samsung nchini China

Kampuni ya simu ya Samsung imezindua rasmi huduma ya malipo ya kutumia simu nchini China kwa ushirikiano na muungano wa wachuuzi nchini humo.

Badala ya kutumia kadi ,huduma hiyo inawaruhusu wateja kutumia simu zao aina ya smartphone kufanya ununuzi.

Soko la kampuni ya China la smartphone likiwa ndilo kubwa duniani linatoa fursa kubwa za biashara kwa mpango wa malipo kupitia simu.

Huduma za malipo za Samsung Pay na Apple Pay zitakabiliwa na ushindani mkubwa na hudma kama hiyo ya Alibaba ambayo kwa sasa inatawala soko la kielektroniki nchini humo.

Mtandao wa WeChat pia una mfumo wa malipo ambao ni maarufu sana nchini China huku kampuni kubwa ya mawasiliano nchini humo Huawei pia ikizindua huduma yake mapema mwezi huu.