EgyptAir: Mtekaji alitumia mkanda bandia wa kujilipua

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mtekaji alitumia mkanda bandia wa mlipuaji wa kujitolea mhanga

Mtekaji mmoja raia wa Misri aliyeilazimu ndege ya EgyptAir kutua nchini Cyprus alitumia ukanda bandia wa mlipuaji wa kujitolea mhanga.

Malengo yake bado hayajabainika lakini rais wa Cyprus alisema kuwa kisa hicho sio kitendo cha kigaidi.

Kanda ya video iliotolewa na waziri wa maswala ya ndani nchini Cyprus ilimuonyesha mtu huyo akipita maeneo kadhaa ya ukaguzi wa kiusalama katika uwanja wa ndege wa Borg El Arab uliopo Alexandria.

Kisa hicho kilikamilika baada ya abiria wote kuachiliwa bila kujeruhiwa katika uwanja wa ndege wa Larnaca huku mtu huyo akijisalimisha.

Maafisa wa Cyprus wamemtaja mtekaji huyo kama Seif Eldin Mustafa na kusema kwamba alikuwa na tatizo la kiakili.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rubani wa ndege ya EgyptAir akitoroka katika ndege hiyo

Waziri wa maswala ya kigeni Loannis Kasoulides amesema Mustafa awali alikuwa ametaka kuzungumza na aliyekuwa mkewe nchini Cyprus ambaye polisi walimleta katika uwanja huo wa ndege kabla ya kutaka mahitaji yasio sahihi.

Maafisa wa polisi mjini Cairo waliwahoji watu wa familia ya Mustafa kulingana na shirika la habari la AP.