Odinga: Magufuli ataifaa Tanzania

Odinga Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania
Image caption Bw Odinga amekuwa kaskazini magharibi mwa Tanzania kwa siku tatu

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga amesema ana imani Rais wa Tanzania John Magufuli ataisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto zinazoikabili.

Bw Odinga amerejea nchini Kenya baada ya kumaliza mapumziko ya siku tatu eneo la Lubambangwe, wilaya ya Chato mkoani Geita, ambako alimtembelea Rais Magufuli ambaye pia yupo mapumzikoni.

Akizungumza katika uwanja wa michezo wa shule ya Sekondari ya Chato kabla ya kuabiri helikopta, Bw Odinga amesema ana imani kuwa Rais Magufuli ataisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo umaskini unaowakabili wananchi wake.

"Lakini mimi najua yeye mwenyewe ana maono, anaona mbele na anajua yale ambayo yanatakiwa yafanyike ili Tanzania iinuke, itoke katika hali ya ufukara na kuwa katika hali ya maendeleo zaidi," amesema Bw Odinga kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu ya Tanzania.

Bw Odinga, ambaye kwa sasa ni kiongozi wa mrengo wa upinzani Kenya, amekuwa rafiki wa karibu wa Dkt Magufuli.

Urafiki wao ulikolea zaidi wawili hao walipokuwa mawaziri wa ujenzi na barabara.