Hisia mseto kuhusu uamuzi wa mahakama ya ICC

Image caption Rais Uhuru Kenyatta wa kenya na viongozi wengine

Vifijo na nderemo vimetanda mji wa Eldoret katika mkoa wa bonde la Ufa nchini Kenya kufuatia uamuzi wa mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC kutangaza kuwa naibu wa rais wa Kenya William Ruto pamoja na mwanahabari Joshua Sang hawana kesi ya kujibu.

Bw Ruto alikabiliwa na mashtaka ya mauaji, kuhamisha watu kwa lazima na mateso yaliyotekelezwa wakati wa vita vya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Mamia ya wakaazi wa eneo hilo walimiminika katika mji wa Eldoret ambao uliathiriwa sana na ghasia hizo siku ya Jumanne ili kusheherekea hatua hiyo.

Wengi waliohojiwa na mwandishi wa BBC Wanyama Chebusiri aliyekuwa katika eneo hilo walikuwa na furaha chungu nzima.

Hata hivvyo waathiriwa wa ghasia hizo ambao hawakutaka majina yao kutajwa walionyesha masikitiko makubwa wakisema kuwa ukweli kuhusu ghasia hizo hautajulikana tena.

Katika taarifa yake baada ya uamuzi huo rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema anajiunga na Wakenya wengine kusheherekea uamuzi huo.

Bw Kenyatta amesema kuwa harakati za kupigania haki hazijakamilika licha ya uamuzi huo na kuongezea kuwa mahakama ya ICC imekuwa ikifanya mambo bila mpangilio, hatua ambayo imewaacha wengi wakingojea kupata haki.

Amesema kuwa serikali yake itaendelea kufanikisha maridhiano, uwiano mbali na kuhakikisha kuwa waathirwa wa ghasia hizo wanapata haki yao.