Kenya yakosa kutii makataa ya WADA

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kenya imeshindwa kutekeleza makataa ya WADA

Kenya imeshindwa kwa mara nyingine kutimiza makataa iliyowekewa na shirikisho la kupambana na matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu mwilini WADA ya kuweka sheria zitakazodhibiti kuenea kwa matumizi ya madawa haya yaliyopigwa marufuku miongoni mwa wanariadha wake.

Hii inafuatia hatua ya bunge la taifa hilo kukosa kupitisha sheria kufikia leo Aprili tarehe 5 ilikuzuia wanariadha wake wasipigwe marufuku ya kushiriki michezo ya Olimpiki.

WADA ilikuwa imeitaka Kenya ipitishe sheria maalum ya kupambana na kuenea kwa madawa hayo haramu.

Aidha wada ilitaka kuundwe kamati maalum itakayoongoza kampeini dhidi ya kuenea kwa madawa hayo haramu na ipewe msingi wa kisheria.

Kamati ya utekelezaji wa kanuni za WADA inakutana baadaye leo huko Montreal Canada na inatarajiwa kupendekeza hatua kuchukuliwa dhidi ya Kenya kwa kushindwa kuratibu sheria za kupambana na madawa hayo haramu.

Haki miliki ya picha b
Image caption Kenya ilishindwa kuratibu sheria ya WADA mwezi Februari.

Iwapo pendekezo la kamati hiyo litakubaliwa na halmashauri kuu ya WADA huenda kauli hiyo ikaratibiwa katika mkutano ujao unaotarajiwa kufanyika May tarehe 12.

Kenya ilishindwa kuratibu sheria ya WADA mwezi Februari.

Kufuatia kushindwa kwa mabingwa hao wa dunia katika riadha kupitisha sheria zitakazoipa uhalali kamati ya kupambana na matumizi ya madawa ya madawa ya kuongeza nguvu mwilini, WADA iliiweka Kenya katika orodha ya mataifa yanayokiuka kanuni zake na ikatoa makataa ya Aprili tarehe 5 (leo).

Wabunge wa Kenya tayari wamelijadili swala hilo bungeni ila wanahitaji kulijadili tena na endapo itapitishwa basi itahitaji sahihi ya rais Uhuru Kenyatta kuifanya iwe sheria.

Daktari Moni Wekesa anayeongoza harakati ya kupambana na madawa ya kuongeza nguvu mwilini anasema kuwa kila kitu ki shwari ni kanuni za bunge na katiba ya nchi tu ndizo zinazochachawiza kupitishwa kwa sheria hiyo mpya.