Mafuriko yaua watu 12 Rwanda

Image caption Mafuriko yaua watu 12 Rwanda

Watu 12 wamefariki dunia na wengine wengi kujeruhiwa kufwatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha nchini Rwanda.

Serikali imewatahadharisha wananchi kuwa ni kipindi cha mvua za El Nino na kuwataka wale wanaoishi katika maeneo yaliyo katika hatari ya kuporomoka na wale wanaoishi katika maeneo ya nyanda chini ambayo huathirika na mafuriko kuhama mara moja.

mwandishi wa BBC aliyeko huko Yves Bucyana anasema kuwa, kulingana na wizara inayohusika na majanga, idadi ya watu waliofariki kutokana na mafuriko imetimia 12.

Wote waliosombwa na mafuriko hayo wanatokeo maeneo ya mji mkuu wa Kigali.

Waziri Seraphine Mukantabana amesema watu wengine 19 walijeruhiwa.

Image caption Waziri Seraphine Mukantabana amesema watu wengine 19 walijeruhiwa.

Aidha anasema kuwa mafuriko hayo yalisababisha hasara kubwa ikiwemo nyumba 149 zilizoporomoka , mbali na barabara na madaraja yaliyoharibiwa.

Familia zilizoachwa bila makao zinaendelea kusaidiwa na serikali.

'' hatua za dharura ni kwamba wamewataka wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyo na hatari kwa maisha ya watu kuhama maeneo hayo mara moja na hata wale wasiojiweza watasaidiwa kuhama ilhali walio na uwezo wametakiwa kuhama mara moja bila masharti.''

Image caption Mafuriko hayo yalisababisha hasara kubwa ikiwemo nyumba 149 zilizoporomoka

Amesema hiki ni kipindi kibaya na kuna hofu vifo zaidi vinawezatokea ikiwa watu hawataitikia mwito wa serikali.

"Ni kipindi cha mvua ya El NiƱo inayoendelea, hivyo hatuna budi kuwataka watu wahame maeneo hatari kwa maisha yao "amesema waziri Mukantabana.

Serikali inasema Rwanda ni nchi ya milima mirefu ambapo ni rahisi kuwa na maporomoko.

Pia ni rahisi mno mafuriko kusomba nyumba zilizojengwa kiholela katika maeneo yenye miinuko; na makazi mengi ya wananchi yanayoporomoka ni yale yalijengwa bila kufwata ramani na taratibu za ujenzi.