Wanajeshi 11 wa TZ watuhumiwa unyanyasaji wa kingono DRC

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mwanajeshi wa umoja wa mataifa

Umoja wa Mataifa unasema kuwa umepokea madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Tanzania mashariki mwa taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Umesema kuwa kumi na moja kati yao wanakabiliwa na madai ya kuwa baba ya watoto na kuna ushahidi wa awali kwamba wengine walifanya ngono na watoto.

Umoja wa Mataifa umetuma kikosi chake katika eneo hilo kuchunguza madai hayo kulingana na ripoti za chombo cha habari cha AP.

Kundi la kwanza la wanajeshi walinda amani wanaotuhumiwa kwa unyanyasaji wa kingono nchini DRC wameshtakiwa kulingana na chombo cha habari cha AFP.

AFP imesema kuwa wanajeshi watatu wa Congo wanaoshtakiwa walikuwa miongoni mwa wanajeshi walinda amani nchini CAR.

Zaidi ya waathiriwa 100 wametoa madai kwamba walinyanyaswa na wanajeshi walinda amani wa Ufaransa.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema kuwa alishtushwa sana na maelezo ya hivi karibuni ya unyanyasaji huo.

AFP inasema kwamba zaidi ya wanajeshi 18 wa DRC wanatuhumiwa na ubakaji ama jaribio la ubakaji dhidi ya raia.