Jaji Mkuu wa Kenya aweka wazi utajiri wake

Mutunga Haki miliki ya picha Willy Mutunga Twitter
Image caption Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga amekuwa akilalamikia kuenea kwa ufisadi

Jaji Mkuu wa Kenya Dkt Willy Mutunga ameweka wazi utajiri wake katika juhudi za kuhimiza uwazi miongoni mwa maafisa wa umma.

Jaji Mutunga amepakia taarifa zake za kutangaza utajiri wake kwenye akaunti yake katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

“Katika kuendeleza maadili ya uwazi na uwajibikaji, ninaweka wazi taarifa za kutangaza utajiri wangu,” ameandika.

“Najua hivi karibuni nitafanyiwa ukaguzi wa maisha yangu na matumizi.”

Kwa mujibu wa nyaraka alizopakia, Jaji Mkuu huyo anaonesha ana mali ya thamani ya shilingi milioni 33 za Kenya ambazo ni sawa na dola za Kimarekani $326,000.

Jaji Mutunga ametoa maelezo kuhusu mshahara wake na kuonesha alilipwa mshahara ghafi wa jumla ya shilingi za Kenya milioni16 ($160,000, £113,000) na akalipa ushuru wa shilingi za Kenya milioni 4.8 ($47,000, £33,000).

Amefafanua pia gharama yake ya maisha na kuonyesha alilipwa marupurupu ya $3,300 (£2,300) wakati wa ziara ya siku 13 aliyoifanya Marekani mwaka 2012.