Afisa wa Mbabazi ajitokeza, asema alijificha Tanzania

Mbabazi Haki miliki ya picha
Image caption Bw Mbabazi alimaliza wa tatu katika uchaguzi uliofanyika 18 Februari

Aliyekuwa meneja wa usalama wa kampeni ya waziri mkuu wa zamani wa Uganda Amama Mbabazi ambaye alidhaniwa kwamba alifariki baada ya kutoweka miezi mitatu iliyopita amejitokeza.

Bw Christopher Aine alijisalimisha kwa nduguye Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Jenerali Salim Saleh.

Bw Aine aliambia kituo cha runinga cha NTV cha Uganda kwamba amekuwa mafichoni jijini Dar es Salaam, Tanzania na kwamba aliamua kuondoka Uganda kutokana na wasiwasi uliotanda baada ya makabiliano ya Ntungamo tarehe 13 Desemba.

Makabiliano hayo yalikuwa kati ya vijana waliovalia fulana za chama tawala cha NRM na waliokuwa wakiimba nyimbo za chama hicho na maafisa wa usalama wa Bw Mbabazi katika wilaya ya Ntungamo, magharibi mwa Uganda.

Bw Aine alitoweka siku mbili baada ya makabiliano hayo.

Amesema alijaribu kuwasiliana na Bw Mbabazi na Mkuu wa Polisi Jenerali Kale Kayihura ili wafanikishe kujitokeza kwake lakini hakufanikiwa kwa sababu aliacha simu zake nyumbani alipoondoka Tanzania.

Serikali ya Uganda iliahidi zawadi ya shilingi 20 milioni za Uganda kwa mtu ambaye angetoa habari ambazo zingesaidia kupatikana kwake.

Jenerali Saleh ameambia wanahabari kwamba Bw Aine atakaa nyumbani kwake yeye akiendelea na mashauriano na serikali kuhakikisha uhuru wake.