Wakuu wanane wa benki Kenya kukamatwa

Chase Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Matawi ya benki ya Chase yamefungwa na benki hiyo kuwekwa chini ya mrasimu

Mkuu wa polisi nchini Kenya ameagiza maafisa wanane wa kuu wa benki nchini Kenya wakamatwe.

Taarifa kutoka kwa mkuu huyo Joseph Boinnet imewataka maafisa sita kutoka kwa Benki ya National na wawili kutoka kwa benki ya Chase wafike kwa polisi kuandikisha taarifa la sivyo wakamatwe.

Maafisa hao wanatuhumiwa kuhusika katika ukiukaji wa maadili.

Benki ya Chase iliwekwa chini ya mrasimu Alhamisi baada ya shughuli katika benki hiyo kukwama kutokana na watu kutoa pesa kwa wingi.

Wateja walianza kuhamisha pesa kutoka kwa benki hiyo baada ya kuenea kwa wasiwasi kuhusu uthabiti wa benki hiyo kifedha. Habari hizo zilienezwa sana kupitia mitandao ya kijamii.

Bw Boinnet amesema mwanamume mmoja amekamatwa kwa “kueneza uongo” kwenye mitandao ya kijamii kuhusu sekta ya benki.

Amewatahadharisha wananchi dhidi ya kusambaza habari kama hizo.

Benki Kuu ya Kenya (CBK) imesema wasiwasi uliotokana na kuenezwa kwa habari za uongozi kuhusu benki ya Chase ndizo zilizopelekea watu wengi kutoa pesa zao Jumatano na kulemaza benki hiyo.

Image caption Dkt Njoroge ameahidi kulainisha sekta ya benki

Gavana wa CBK Dkt Patrick Njoroge amekuwa akikabiliana na maafisa walio waadilifu katika sekta ya benki nchini Kenya tangu kuchukua usukani.

"Hatuwezi kuwavumilia maafisa wa benki ambao ni wahuni, wale wanaoiba kutoka kwa watu wanaoweka akiba pesa zao,” Dkt Njoroge amenukuliwa na shirika la habari la Reuters.

Jumatano, benki ya Chase ilimsimamisha kazi mwenyekiti wake na meneja mkurugenzi baada ya kutolewa kwa taarifa mbili kinzani za matokeo ya kifedha.

Moja ilishusha mikopo iliyochukuliwa na maafisa wa ndani wa benki hiyo. Nyingine ilionyesha wakurugenzi walikuwa wamekopeshwa $80m, na mikopo isiyolipwa katika benki hiyo ilikuwa imepanda na kufika $100m.

Mnamo 29 Machi, Benki ya National iliwatuma kwenye likizo ya lazima afisa mkuu mtendaji na mameneja watano wakuu kupisha ukaguzi wa kifedha katika benki hiyo.