Uber yakubali kulipa $10m kumaliza kesi

Uber Haki miliki ya picha Getty
Image caption Uber hutumia mfumo tofauti kuwachunguza madereva

Kampuni ya magari ya teksi ya Uber imekubali kulipa $10m (£7m) kumaliza kesi kuhusu upekuzi wa habari kuhusu historia ya madereva wao jimbo la California, Marekani.

Uber ilishtakiwa mwaka 2014 baada ya kudai kwamba utaratibu wake wa kuwachunguza madereva wake ulikuwa bora kushinda uliotumiwa na magari ya teksi ya kawaida.

Lakini viongozi wa mashtaka San Francisco na Los Angeles walisema tangazao la Uber, lililowalenga kuwafanya wananchi waamini ilikuwa salama zaidi kuliko washindani wake, lilikuwa la kupotosha.

Tofauti na kampuni za kawaida za teksi, Uber huwa haitumii alama za vidole za madereva kuchunguza historia yao. Njia hiyo huwa inasaidia kubaini iwapo mtu fulani amewahi kushtakiwa au kupatikana na makosa.

Badala yake, Uber hutumia hazina data nyingine kuhusu wahalifu kuwachunguza madereva wake. Hazina data hiyo ina takwimu za miaka saba kwenda nyuma.

Kama sehemu ya makubaliano ya kumalizwa kwa kesi, Uber imesema haitakuwa itumia maneno kama „teksi salama zaidi barabarani” kwenye matangazo yake.

Viongozi wa mashtaka walisema Uber ilishindwa kuzuia watu 25 waliopatikana na makosa ya uhalifu awali kuwa madereva wake. Baadhi walipatikana na makosa ya unyanyasaji wa kingono na kulikuwa na mmoja aliyepatikana na kosa la mauaji.

"Ajali na visa hutokea wakati mwingine,” Uber ilisema kupitia taarifa.

Uber italipa $10m katika kipindi cha siku 60 ambazo zitagawanywa kwa kiasi sawa baina ya serikali za San Francisco na Los Angeles.

Kampuni hiyo ikishindwa kutimiza masharti hayo, basi italazimika kulipa $15m zaidi katika kipindi cha miaka miwili.