FIFA yatishia kuipiga marufuku Nigeria

Image caption FIFA yatishia kuipiga marufuku Nigeria

Shirikisho la kandanda duniani limetishia kuipiga marufuku Nigeria kutoka kwenye mashindano yeyote ya kimataifa iwapo haitamrejesha afisini rais wa NFF Amaju Pinnick mara moja.

Rais wa NFF Amaju Pinnick aliondolewa madarakani Alhamisi iliyopita baada ya mahakama moja ya Jos kuamua kuwa kiongozi wa sasa Pinnick alishindwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka wa 2014.

Mahakama ilisema kuwa Chris Giwa ndiye anayefaa kuwa rais wa shirikisho la soka la Nigeria NFF.

FIFA imeonya kuwa Nigeria imo katika hatari ya kupigwa marufuku endapo itatekeleza uamuzi wa mahakama.

Katika taarifa iliyotumwa kwa serikali ya Nigeria Jumatatu tarehe 11 Aprili kaimu katibu wa FIFA Markus Kattner, anasema uamuzi huo wa mahakama unatafsiriwa kama kuingiliwa kati kwa maswala ya kandana.

''Bila shaka uamuzi wa mahakama hiyo ya Jos unafasiriwa kuwa ni kuhitilafu uendeshaji wa shirikisho na hiyo bila shaka inakiuka kanuni za FIFA ambazo haziruhusu maswala ya kandanda kuamuliwa mahakamani.'' alisema bw Kattner.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption FIFA imeonya kuwa Nigeria imo katika hatari ya kupigwa marufuku endapo itatekeleza uamuzi wa mahakama.

Hii sio mara ya kanza kwa bw Chris Giwa kwenda mahakamani kutafuta suluhu ya mgogoro wa usimamizi wa shirikisho la kandanda la Nigeria.

Mwaka uliopita pia alikwenda katika mahakama ya michezo ambapo alishindwa katika uamuzi uliotolewa Mei tarehe 18 2015.

Tofauti hizo zinaiweka timu ya Olimpiki ya Nigeria Super Eagles katika hatari kubwa ya kupigwa marufuku kutoka mashindano hayo yatakayofanyika huko Rio de Jenairo na vilevile kuhujumu maandalizi yao ya kipute cha dunia cha mwaka wa 2018.