Kerry azuru makumbusho ya Hiroshima

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kerry akiwa na mawaziri wengine mjini Hiroshima

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni nchini Marekani amefanya ziara ya kihistoria katika eneo la makumbusho la Hiroshima nchini Japan ambapo lilifanyika shambulizi la kwanza la bomu la nuklia.

Kerry ndiye waziri wa kwanza wa mashauri ya nchi za kigeni wa marekani kuwai kufanya ziara mjini Hiroshima ambapo karibu watu 140,000 waliuawa wakati Marekani ilidondosha bomu la nuklia mwaka 1945.

Kerry aliungana na mawaziri kutoka nchi za G7 ambao walikuwa wakifanya mazungumzo mjini humo. Waliweka shada la maua katika eneo la makumbusho na kukaa kimya kwa dakika moja.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mosji ulitokana na shambulizi hilo la nuklia

Mawaziri hao pia walizuru eneo ambapo bomu hilo lilipuka pamoja na eneo la makumbusho lililo karibu linaloelezea historia za watu walioangamia.

Mnamo tarehe 6 mwezi Agosti mwaka 1945 mwendo wa saa 08:10 saa za Japan, ndege aina ya B-29 bomber ilidondosha bomu lililopewa jina "Little Boy" mjini Hiroshima.

Karibu watu 70,000 waliaga dunia papo hapo. Takriban watu 140,000 walikuwa wameaga dunia wakati mwaka ukiisha kutokana na majeraha na athari za mionzi ya bomu hilo.