Bomba la mafuta Afrika Mashariki lajadiliwa Uganda

M7 Haki miliki ya picha Uhuru Kenyatta Facebook
Image caption Rais Museveni alikutana na Rais Kenyatta Nairobi

Mkutano unaohusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi Bahari ya Hindi umeanza mjini Kampala nchini Uganda.

Mkutano huu unayashirikisha mataifa waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki - Kenya, Uganda na Tanzania - ambapo baada ya siku tatu maafisa wa Serikali kutoka mataifa hayo wataamua iwapo Bomba hilo linafaa kutoka Uganda na kupitia nchini Tanzania hadi Bandari ya Tanga au kupitia Kenya hadi Bandari ya Lamu au Bandari ya Mombasa.

Bomba la kutoka Tanga hadi Uganda litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima eneo la ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Bomba la kutoka Hoima na kwenda Lokichar kisha hadi Lamu linakuwa na urefu wa kilomita 1,476.

Pendekezo la kutoa mafuta Lokichar pamoja kisha kupitia Hoima nchini Uganda na kufika Tanga itakuwa na urefu wa kilomita 2,028.

Ingawa ripoti itakayojadiliwa imetoa njia tatu zinazoweza kutumiwa, ni dhahiri kuwa Kenya na Tanzania watakuwa katika hali ya kuchunguzana sana.

Mazungumzo ya mwezi mmoja uliopita kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Rais Museveni na wakati huo huo kati ya Rais Museveni tena na Rais John Pombe Magufuli juu ya swala la bomba la kupeleka mafuta hadi Bahari ya Hindi yamezusha uhasama baridi kati ya Kenya na Tanzania.

Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania
Image caption Rais Magufuli akiwa na Rais Museveni

Tayari vyombo vya habari nchini Tanzania vimesema kuwa Rais Magufuli na Rais Museveni washatia sahihi bomba hilo lipitie Tanzania hadi Bandari ya Tanga.

Mkutano uliofanyika nchini Kenya kati ya Rais Kenyatta na Rais Museveni juu ya bomba hilo, kufuatia mwaliko wa Rais Kenyatta, ulimalizika majuma machache yaliyopita bila suluhu yoyote.

Kila taifa hilo lina hamu ya kuhakikisha bomba la mafuta linapitia kwake kutokana na manufaa ya kiuchumi.

Mafuta ghafi ya Kenya hayako mbali sana na yale ya Uganda lakini ni wazi kwamba kuwa na bomba nchini ni biashara ya kipekee inayoleta faida zaidi.