Watu 5 wauawa Ruyigi Burundi

Haki miliki ya picha GETTY
Image caption Watu 5 wauawa Ruyigi Burundi

Watu waliojihami kwa bunduki wamewaua watu watano na kuwajeruhi wengine saba walipofyatua risasi katika soko moja iliyoko Mashariki mwa eneno la Ruyigi nchini Burundi.

Hili ni shambulio la hivi karibuni katika nchi hiyo ambayo imekumbwa na msururu wa mauaji.

Abdalla Hassan ambaye ni mkuu wa mkoa wa eneno hilo la Ruyigi ametaja mauaji hayo kuwa uhalifu wa kivita kwani waliwashambulia raia wasiokuwa na hatia wala silaha.

''Kama kweli hawa watu walikusudia kupigana si basi wangelikwenda kwenye kituo cha polisi ama cha jeshi wakashambulie?

Mbona wanawashambulia wananchi maskini ambao hata silaha hawana ,wamekosa nini ? aliuliza bw Hassan.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Burundi imejipata katika mzozo wa kisiasa tangu rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kutangaza nia ya kuwania urais kwa muhula wa tatu.

Burundi imejipata katika mzozo wa kisiasa tangu rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kutangaza nia ya kuwania urais kwa muhula wa tatu.

Wakosoaji wake wanasema kuwa hicho ni kinyume cha sheria na kuwa alikuwa anakiuka katiba ya nchi.

Zaidi ya watu 400 wameripotiwa kuuawa katika machafuko yaliyofuatia uteuzi na kisha uchaguzi wa Nkurunziza.

Zaidi ya watu laki mbili u nusu wametorokea mataifa jirani wakihofia umwagikaji wa damu.