Hasara yaiporomosha ndege ya Senegal

Image caption Shirika la ndege la Senegal kufungwa kufuatia hasara kubwa.

Shirika la ndege la Senegal kufungwa kufuatia hasara kubwa.

Mamlaka kuu nchini Senegal imetangaza kuwa kampuni yake kuu ya ndege itaondolewa na nyingine mpya kuwekwa, katika muda wa majuma machache yajayo.

Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa mamlaka kuu ya udhibiti wa safari za ndege, kuipokonya barua na cheti chake cha kufanyia kazi, kampuni ya Senegal Airlines.

Yamkini shirika hilo la ndege la Senegal limepata hasara kubwa na inadaiwa kope si zake.

Aidha serikali inalaumu usimamizi mbaya kwa kuporomoka kwa shirika hilo la ndege.

Waziri wa fedha wa Senegal, Ahmadou Ba, alitangaza hayo bila ya kutoa taarifa ya kina kuihusu kampuni hiyo mpya ya ndege ambayo itachukua mahala pa kampuni ya sasa ya safari za ndege nchini humo ambayo imelemazwa na madeni.

Senegal Airlines, ilibuniwa mnamo mwaka 2009, ina madeni yanayofikia dola milioni 78 za kimarekani iliyopewa na wakopeshaji wake.

Viongozi wa vyama vya kuwatetea wafanyikazi wapatao 229, wanasema kuwa wafanyikazi hao wa kampuni hiyo hawajalipwa mishahara kwa miezi kadhaa.

Image caption Shirika la ndege la Kenya pia lilitangaza hasara ya dola milioni 25 na sasa inajiandaa kuwafuta kazi takriban wafanyikazi 600.

Wawekezaji wa kibinafsi wanamiliki asilimia 64 ya kampuni hiyo ilihali asilimia iliyosalia ikimilikiwa na serikali.

Mashirika kadhaa ya ndege barani Afrika yamekuwa na kipindi kibaya katika miaka ya hivi karibuni baada ya mashirika makubwa makubwa ya ndege kuanza kulenga Afrika na hivyo kupunguza kitega uchumi cha mashirika ya bara la Afrika.

Mwezi uliopita shirika la ndege la Cape verde lilitangaza nia ya kupunguza idadi ya wafanyi kazi wake na pia safari za ndege.

Vilevile shirika la ndege la Kenya pia lilitangaza hasara ya dola milioni 25 na sasa inajiandaa kuwafuta kazi takriban wafanyikazi 600.