Polisi wa Chicago ni wabaguzi, uchunguzi wabaini

Maandamano Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wakazi wamekuwa wakiandamana kupinga mauaji yanayotekelezwa na polisi

Polisi katika mji wa Chicago nchini Marekani wamejawa na ubaguzi wa rangi, imesema ripoti mpya rasmi.

Ripoti hiyo imetayarishwa na jopo maalum lililoundwa kutokana na ghadhabu ya umma baada ya polisi kulaumiwa kwa kuwapiga risasi kiholela raia wasio Wazungu.

Jopo hilo limesema polisi waliwalenga watu weusi na jamii ya Latino na hutumia nguvu kupita kiasi kukabiliana nao.

Ripoti hii imependekeza mageuzi 100.

Asilimia 74 ya mamia ya watu waliouawa na maafisa wa polisi walikuwa raia weusi, licha ya kwamba idadi ya watu weusi ni asilimia 33 pekee.

Idara ya polisi mjini Chicago ndiyo ya tatu kwa ukubwa nchini Marekani.

Aidha visa vya mauaji katika mji huo vilipanda kwa asilimia 84 mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Haki miliki ya picha Getty

Kulizuka maandamano ya umma pale afisa wa polisi Mzungu alipompiga risasi na kumuua kijana mweusi.

Maandamano hayo yalichochea Wizara ya Haki ya Marekani kuanzisha uchunguzi dhidi ya mauaji hayo.