Polisi Mwarabu apewa cheo cha juu Israel

Jamal Hakrush Haki miliki ya picha AP
Image caption Hakrush alipandishwa cheo rasmi Jumatano

Afisa wa polisi wa Kiarabu amepewa cheo cha juu zaidi kuwahi kupewa Mwislamu katika idara ya polisi nchini Israel.

Jamal Hakrush amepewa cheo cha naibu kamishna wa polisi baada ya miezi kadhaa ya vita kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Atasimamia maswala ya polisi katika jamii za Kiarabu ambapo kumekuwa na kutoaminiana baina ya raia na polisi kwa miaka mingi.

Katika kila Waisraeli watano, mmoja huwa Mwarabu na Waarabu hao hulalamika mara kwa mara kwamba serikali huwa haijali usalama wao na hupokea huduma duni.

Malalamiko hayo yameungwa mkono na shirika la kupigania haki za kinadamu la Human Rights Watch ambalo hapo awali lilikuwa limechapisha ripoti kadhaa zikigusia ubaguzi, ambao Waarabu wamekuwwa wakikumbana nao.

Naibu Kamishna, Hakrush, anayetoka kijiji cha Galilee, eneo la Kafr Kanna, ataongoza kitengo cha polisi wapya walioteuliwa hivi majuzi ili kuimarisha usalama katika jamii ya Waarabu, gazeti la The Times Of Israel limeripoti.

Hakrush alikabidhiwa rasmi wadhifa wake mpya siku ya Jumatano katika sherehe iliyohudhuriwa na kamishna wa polisi Roni Alsheich.

Moja ya majukumu yao yatakuwa kuzuia silaha haramu kuwafikia Waarabu.

Bw Alsheich, pia anataka kupunguza dhuluma za kinyumbani, visa vya mauaji na aina nyingine za uhalifu maeneo ya Waarabu.

Amesema serikali inataka kuteuwa maafisa wapya 1,300 na kujenga vituo vipya vya polisi katika maeneo wanamoishi Waarabu.