Helikopta ilivyobeba pochi ya gavana Marekani

Robert Bentley Haki miliki ya picha AP
Image caption Robert Bentley anasema hakutenda kosa lolote

Helikopta ya polisi ilitumwa kuchukua pochi ya gavana wa jimbo moja nchini Marekani, safari iliyogharimu $4,000 (£2,800), uchunguzi umebaini.

Kisa hicho kilitokea mwishoni mwa 2014.

Gavana wa Alabama Robert Bentley aliondoka Tuscaloosa kuelekea kwenye nyumba yake ya ufukweni, mwendo wa saa tano hivi ukitumia gari, lakini akasahau pochi yake.

Aliwataka maafisa wake wa usalama kwenda kuchukua pochi hiyo. Maafisa hao walitumia helikopta hiyo ya polisi, rekodi za safari za ndege zimeonesha.

Bw Bentley anakabiliwa na shinikizo za kumtaka ajiuzulu kutokana na sakata ya unyanyasaji wa kingono.

Lakini anasema hakuagiza ndege itumiwe kwenda kuchukua pochi.

"Niliwaomba tu waende wakachukue pochi yangu, sikuwaambia watumie njia gani,” gavana huyo ameambia mtandao wa AL.com.

„Sikuwaambia watumie helikopta. Ni lazima uwe na pochi yako kwa sababu za kiusalama. Mimi ni gavana. Na ni lazima niwe na pesa. Ni lazima ningenunua kitu cha kula. Na nilihitaji vitambulisho vyangu.”

Tovuti ya AL.com inasema safari hiyo ya helikopta iligharimu mlipa kodi takriban $4,000 (£2,800).