Tunisia yaonya nchi za kigeni zisiingilie Libya

Essebsi Haki miliki ya picha AP
Image caption Bw Essebsi amesema huenda migawanyiko zaidi ikazuka

Rais wa Tunisia Beji Caid Essebsi ameyatahadharisha mataifa ya kigeni dhidi ya kuingilia kijeshi katika nchi jirani ya Libya.

Katika mahojiano na BBC, Bw Essebsi amesema hatua kama hiyo inaweza kugawanya zaidi taifa hilo lililozama katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Amesema hayo huku wasiwasi ukiendelea kuongezeka miongoni mwa nchi za Magharibi kuhusu kuenea kwa kundi la Islamic State nchini humo.

Majuzi, Rais wa Marekani Barack Obama alisema wapiganaji wengi wanaingia Libya kutokana na operesheni kali inayoendeshwa Syria na Iraq.

Inadaiwa majeshi ya nchi wanachama wa shirika la kujihami la Nato yamekuwa yakiandaa mpango wa kutuma wanajeshi Libya iwapo yataombwa kufanya hivyo na serikali mpya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.