Mwanamuziki afuta tamasha baada ya mbwa kuugua

Stone Haki miliki ya picha
Image caption Stone anatumai ataweza kutumbuiza mashabiki wake Venezuela

Mwanamuziki mmoja kutoka Uingereza ameahirisha tamasha yake ya muziki visiwa vya Caribbean baada ya mbwa wake kuugua.

Joss Stone alisema mbwa huyo kwa jina Missy ni kama mtoto kwake.

Aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba aliahirisha tamasha ya Jumamosi kisiwa cha Barbados na Jumanne kisiwa cha Trinidad baada ya mbwa wake kuanza kuvuja damu.

“Najua linaonekana kama jambo la kushangaza lakini kwangu mbwa huyu ni kila kitu,” aliongeza.

“Nawaahidi nitarejea, lakini kwa sasa Missy yuko mbele ya mambo mengine yote,” aliandika.

Amesema anatumai kufanya onesho nchini Venezuela tarehe 21 Aprili mambo yakiwa sawa.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Stone akitumbuiza awali

Stone tayari ameandaa maonesho India, Nepal, Panama na Costa Rica kama sehemu ya safari yake nchi mbalimbali duniani kuvumisha albamu yake ya saba kwa jina Water For The Soul.