Mazungumzo kuhusu Burundi kufanyika Tanzania

Burundi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Watu karibu 500 wameuawa nchini Burundi tangu Aprili mwaka jana

Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa ametangaza kwamba kikao cha kwanza cha mazungumzo ya kutafuta amani nchini Burundi kitafanyika wiki ijayo.

Bw Mkapa aliteuliwa na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki mapema mwezi uliopita kuwa mfanikishi wa mazungumzo ya kutatua mzozo wa kisiasa katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisalia kuwa mpatanishi mkuu.

Mazungumzo ya kutafuta amani yalifeli mwishoni mwa mwaka jana baada ya upande wa serikali kusema hauwezi kuzungumza na watu waliohusika kwa njia moja au nyingine katika jaribio la mapinduzi la mwezi Mei mwaka jana.

Bw Mkapa ameandika kwenye Twitter kwamba wadau wote wanatarajia kuhudhuria kikao cha kwanza cha mazungumzo ambacho kitafanyika mjini Arusha kuanzia tarehe 2 Mei hadi 6 Mei.

"Nimepata idhini kutoka kwa Rais wangu, kikao changu cha kwanza cha Mashauriano ya Burundi kitakuwa mjini Arusha,” aliandika.

Ukosefu wa usalama umeendelea kuwa tatizo kuu nchini Burundi na visa vya watu kuuawa kiholela vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara.

Tulifikaje hapa?

  • Aprili 2015: Ghasia zazuka baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza atawania urais kwa muhula wa tatu.
  • Mei 2015: Mahakama ya Kikatiba yaunga mkono hatua ya Nkurunziza kuwania. Maelfu ya raia watoroka huku maandamano yakiendelea.
  • Mei 2015: Maafisa kadha wa jeshi wafanya jaribio la kupindua serikali. Jaribio lafeli.
  • Julai 2015: Uchaguzi wafanyika, na Bw Nkurunziza kutangazwa mshindi. Upinzani wapinga matokeo huku kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa akisema uchaguzi huo ulikuwa “mzaha”.
  • Desemba 2015: Watu 87 wauawa baada ya wanajeshi kujibu mashambulio yaliyotekelezwa katika vituo vya jeshi Bujumbura
  • Januari 2016: Madai ya kuwepo kwa makaburi ya pamoja yaibuka. Maafisa wa usalama wa Burundi watuhumiwa kutekeleza ubakaji wakikabiliana na wapinzani.
  • Aprili 2016: Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi lasema wakimbizi 250, 000 wametoroka Burundi na kukimbilia nchi jirani.
  • Aprili 2016: ICC yaanzisha uchunguzi wa awali kuhusu mauaji, dhuluma, ubakaji na kutoweka kwa watu Burundi.