Mwanasiasa wa miaka 90 kuoa mwanamume Marekani

Harris Wofford Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wofford alifiwa na mkewe Clare miaka 20 iliyopita

Seneta mmoja wa zamani wa Marekani, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 90, ametangaza kwamba atamuoa mwanamume wa umri wa miaka 40.

Wawili hao watafunga ndoa mwishoni mwa mwezi huu.

Harris Wofford, aliyehudumu katika utawala wa Rais J F Kennedy kama msaidizi maalum aliyehusika na masuala ya haki za raia, aliachwa akiwa mjane baada ya mkewe Clare kufariki kutokana na saratani ya damu miaka 20 iliyopita.

Walikuwa wameishi katika maisha ya ndoa kwa miaka 48.

Akiandika katika gazeti la New York Times, Bw Wofford amesema anajihisi mwenye bahati sana kuishi katika enzi ambazo Mahakama ya Juu Marekani imetambua kwamba “ndoa haitegemeu maumbile ya mtu kijinsia, uamuzi au ndoto za mtu.”

“Msingi wake ni upendo.”

Mwanamume atakayeolewa naye ametambuliwa kama Matthew Charlton.

Wofford alihudumu wakati mmoja kama seneta wa chama cha Democratic akiwakilisha jimbo la Pennsylvania.

Aidha, alihudumu kama mshauri wa Dkt Martin Luther King Jr.

"Mnamo Aprili 30, katika umri wa miaka 90 na 40, tutaunganisha mikono yetu, tukiapa kuunganizhwa pamoja (kwenye ndoa): kuwa pamoja na kuishi pamoja, kwa mema na kwa mabaya, kwa utajiri na umaskini, katika maradhi na katika afya bora, kupenda na kuenzi, tangu kifo kitutenganishe," amehitimisha Wofford katika makala yake iliyochapishwa katika gazeti la New York Times Jumapili.