Benki ya Chase ilivyovuma kisha ikayumba Kenya

Benki
Image caption Benki ya Chase itafunguliwa Jumatano

Benki ya Chase Bank itafunguliwa tena Jumatano baada ya kufungwa kwa takriban wiki tatu.

Lakini, nini hasa kilienda kombo katika benki hiyo?

2015: Ilikuwa yafanya vyema sana

Kampuni ya uhasibu ya Deloitte iliipokeza tuzo ya kampuni bora zaidi ya kufanyia kazi. Kadhalika, ilipokezwa tuzo ya Kampuni Iliyofanya Vyema Zaidi.

Ni benki ya aina gani?

Ilianzishwa 1996, na kubadilisha mkakati wake ikiangazia sana wafanyabiashara wadogo wadogo.

Ilijizolea sifa kama benki yenye uhusiano mwema sana na siku zilivyozidi kusonga, iliunda uhusiano wa karibu sana na wateja wake.

2016: Walioweka pesa kwenye benki hiyo ni pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo 27,000 na vyama vya akiba na mikopo 147 vyenye wanachama karibu 1.3 milioni.

Mzozo: Aprili 7 2016

Walioweka pesa kwenye benki walipokea habari kwamba benki hiyo ilikuwa imefichua mabilioni ya pesa yaliyokuwa yamekopeshwa wakufugenzi na wafanyakazi wa benki hiyo. Mikopo hii haikuwa imefichuliwa awali kwenye taarifa za kifedha.

Wateja wengi walifika katika matawi ya benki hiyo wakitaka kutoa pesa zao. Siku ya kwanza baadhi walifanikiwa lakini baada ya muda benki ilizidiwa na ikafungwa.

Benki Kuu ya Kenya (CBK) iliweka benki hiyo chini ya mrasimu ikisema Chase Bank ilikuwa imeshindwa kutimiza baadhi ya majukumu yake ya kifedha.

Chase Bank ndiyo benki ya tatu kuwekwa chini ya mrasimu katika kipindi cha miezi tisa Kenya baada ya benki benki ya Imperial Bank iliyofungwa Oktoba na benki ya Dubai iliyofungwa mwezi Agosti.

Sakata: Mikopo ya ndani

Chase Bank ilitoa mikopo ya Sh16.6 bilioni ($158 milioni) kwa watu binafsi na taasisi mbalimbali zilizokuwa na uhusiano na wakurugenzi au wafanyakazi wa benki hiyo, bila dhamana inayohitajika.

Mkurugenzi mmoja alijikopesha jumla ya Sh7.9 bilioni ( $ 7 milioni), nyingi bila dhamana na kwa kuzidi viwango vinavyohitajika. Mkurugenzi huyo alijikopesha zaidi ya asilimia 25 ya jumla ya mtaji, kiwango kilichowekwa kwenye Sheria ya Benki.

Sh8.7 bilioni( $ 8 milioni) huenda zisipatikane tena ikizingatiwa kwamba hazikuwa zinalipwa inavyohitajika kila mwezi au waliozikopa hawakutoa stakabadhi za kutosha.

Nani wa kulaumiwa?

“Benki hiyo ilikabiliwa na matatizo ya kupata pesa za kutosha kuwapa wateja wake kutokana na habari zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii,” gavana benki kuu Dkt Patrick Njoroge alisema.

LAKINI

Mamlaka ya Masoko ya Mtaji (CMA) ilikosolewa kwa sababu ilikuwa imeidhinisha kuuzwa kwa hati fungani ya Sh10 bilioni ($10 milioni) – Sh4.8 bilioni ( $4 milioni) ambayo iliuzwa, licha ya mapungufu yaliyojitokeza sasa ya uongozi katika benki hiyo.

Wakaguzi wa hesabu za benki hiyo Deloitte East Africa pia hawakuweza kuthibitisha iwapo taarifa za matokeo ya kifedha ya benki hiyo zilikuwa sahihi.

Chase Bank inafunguliwa tena tarehe 27 Aprili 2016

Benki ya Kenya Commercial Bank iliteuliwa kusimamia Chase Bank chini ya makubaliano kwamba maalum.

Watu wataweka pesa au watakimbia kuzitoa?

Wateja wataweza kupata pesa walizoweka amana, kiwango cha juu zaidi kikiwa Sh1 milioni($10,000) punde baada ya benki kufunguliwa, CBK ilisema.

“Wateja wa Chase Bank wataweza kufikia amana zao kufikia hadi Sh1 milioni,” CBK ilisema.

Takwimu: Jumla ya akaunti 167,290, ni asilimia 97 ya akaunti zote na zina asilimia sita pekee ya amana. Wenye akaunti hizi wataweza kupata pesa zao zote.