Maandamano makubwa yatarajiwa Baghdad

Sadr Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Al-Sadr ana ushawishi mkubwa Iraq

Maandamano makubwa yanatarajiwa kufanyika leo katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Hatua hiyo inatokana na mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini humo pamoja na kukosekana kwa mabadiliko katika sera ya taifa.

Maandamano hayo yaliyoitishwa na kiongozi mmoja wa madhehebu ya Kishia na ambaye ana ushawishi mkubwa Moqtada al-Sadr yanatokea wakati amabapo Bunge la Iraq linajaribu kupiga kura kuidhinisha baraza jipya la mawaziri baada ya uhasama ulioshuhudiwa kwa wiki tatu sasa.

Waziri mkuu, Haider al-Abadi, amelitaka baraza la mawaziri la sasa ambalo lilibuniwa chini ya vyama vidogo vidogo vya kisiasa, kuondolewa na baraza jingine jipya libuniwe lenye watu walio na ujuzi wa sheria, kama mojawepo ya vigezo vya mfumo wake mpya wa kuiletea nchi hiyo mageuzi yafaayo.

Mwaandishi wa BBC mjini Baghdad anasema kuwa huu ndio mgogoro mbaya sana wa kisiasa nchini Iraq tangu kuangushwa kwa utawala wa Saddam Hussein mnamo mwaka wa 2003.