George Weah kuwania tena urais Liberia

Weah Haki miliki ya picha AFP
Image caption Weah aliwania urais 2005 lakini akashindwa na Sirleaf

Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Liberia George Weah ametangaza kwamba atawaniua urais wka mara ya pili.

Amesema bado ana ndoto ya kubadilisha taifa hilo.

Bw Weah, alichezea klabu kubwa kama vile Paris Saint-Germain, AC Milan na Chelsea, na alikuwa mchezaji Mwafrika aliyekuwa juu zaidi kwenye orodha ya Fifa ya wachezaji stadi zaidi wa karne ya 20.

Aliwania urais mara ya kwanza 2005 lakini akashindwa na rais wa sasa Ellen Johnson Sirleaf.

Muhula wa pili wa Rais Sirleaf utamalizika 2017 na chini ya katiba ya nchi hiyo hawezi kuwania tena.

Wakati wa uchezaji wake, Weah alikuwa balozi mwema wa UN.

Baadaye alijiingiza katika siasa. Amekuwa akihudumu kama seneta wa mkoa wa Montserrado magharibi mwa nchi hiyo. Mkoa huo unajumuisha pia mji mkuu wa Monrovia.

Mwaka 2011 alikuwa mgombea mwenza wa Winston Tubman lakini hawakushinda.

Bw Weah ni wa chama cha upinzani cha Congress for Democratic Change (CDC).