Mtaalamu aliyejiita Nakamoto ajitambulisha

Wright
Image caption Wright amesema yeye hataki sifa

Mjasiriamali mashuhuri nchini Australia Craig Wright amejitambulisha hadharani kwamba ndiye Satoshi Nakamoto aliyevumbua teknolojia mashuhuri ya sarafu ya mtandaoni ijulikanayo kama Bitcoin.

Tangazo lake limefikisha kikomo kipindi cha uvumi na suitafahamu kuhusu nani hasa aliyeanzisha mfumo huo wa sarafu ambao ni maarufu sana.

Bw Wright ametoa ushahidi wa kiteknolojia akitumia sarafu za Bitcoin zinazoaminika kumilikiwa na mwanzilishi wa Bitcoin.

Wanachama mashuhuri wa jamii inayotumia Bitcoin pamoja na wataalamu wakuu waliosaidia kuunda na kuendeleza sarafu hiyo pia wamethibitisha madai ya Bw Wright.

Bw Wright amefichua utambulisho wake kwa mashirika matatu ya habari - BBC, Economist na GQ.

Alipokutana na BBC, Bw Wright aliweka saini ujumbe wake akitumia ufunguo wa kufunga ujumbe ambao ulitumiwa nyakati za kwanza za kustawishwa kwa sarafu ya Bitcoin.

Ufunguo huo ulihusishwa sana na sarafu za bitcoin ambazo zinaaminika kuundwa na Satoshi Nakamoto.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wright alimtumia Finney bitcoin mara ya kwanza 2009

"Ndizo nguzo zilizotumiwa kutuma sarafu 10 za bitcoin kwa Hal Finney mwezi Januari (2009) kama shughuli ya kwanza ya kibiashara kufanywa kwa kutumia bitcoin,” amesema Bw Wright akijidhihirisha kwamba ndiye Nakamoto.

Mtaalamu Hal Finney ni mmoja wa wahandisi waliosaidia sana kukuza wazo la Bw Wright la sarafu hiyo.

“Ninataka kundelea kufanya kile ninachofanya na hilo ndilo nitafanya. Na sifanyi kazi na kuvumbua na kuandika karatasi za kisomi na programu za kompyuta kwa kutokea mbele ya televisheni. Sitaki pesa na sitaki sifa, sitaki kutukuzwa, ninataka kuachwa peke yangu,” amesema.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Bitcoin hutumiwa sana duniani

Bitcoin zimetambuliwa kama sarafu na mashirika mengi na hutumiwa kulipia bidhaa na huduma – kuanzia kwa kusafirisha pesa kutoka nchi moja hadi nyingine hadi kulipa kikombozi kupata tena data iliyofungwa na virusi vya kompyuta.

Kwa sasa kuna sarafu karibu 15.5 milioni za bitcoin duniani.

Kila moja na thamani ya takriban $449 (£306).

Satoshi Nakamoto anaaminika kumiliki bitcoin karibu milioni moja ambazo akiziuza zinaweza kumzolea karibu $450m.