Waliofariki mkasa wa jengo Nairobi wafika 21

Huruma
Image caption Watu 90 bado hawajulikani walipo

Idadi ya watu waliofariki baada ya jengo la ghorofa sita kuporomoka Nairobi imefika 21 baada ya miili mingine mitano kufukuliwa kutoka kwenye vifusi.

Waokoaji wamewanusuru watu 135 huku wengine zaidi ya 90 wakiwa bado hawajulikani walipo.

Inahofiwa wamefukiwa kwenye vifusi vya jengo hilo lililoporomoka katika mtaa wa Huruma kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.

Msemaji wa polisi Charles Owino ameambia BBC kwamba mwenye jengo hilo kwa sasa yumo korokoroni na anahojiwa kuhusu mkasa huo. Maafisa wa serikali ya jimbo la Nairobi walikuwa wamepiga marufuku jengo hilo mapema na kusema halifai kuwa makazi ya binadamu.

Image caption Waokoaji wanaendelea kuwatafuta manusura

Ingawa juhudi za uokoaji zinaendelea, watoaji wa misaada wanahofu kwamba huenda manusura walionaswa kwenye vifusi vya jengo hilo wasipatikane wakiwa hai kutokana na hali mbaya ya hewa.

Watabiri wa hali ya hewa wameonya kwamba mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini Kenya hasa mjini Nairobi itaendelea kwa siku chache zijazo.