Mvumbuzi wa PIN alivyoondoka mikono mitupu

PIN Haki miliki ya picha PA
Image caption Goodfellow alivumbua PIN miaka 50 iliyopita

Je, wajua mtu aliyevumbua nambari ya siri maarufu kama PIN ambayo watu wengi hutumia katika kadi za benki na katika kufanya malipo hakulipwa chochote kutokana na uvumbuzi wake?

Mwanamume huyo si mwingine ila ni James Goodfellow.

Alipata wazo la kutumiwa kwa nambari za siri kulinda akaunti za benki siku kama ya leo miaka 50 iliyopita.

Uvumbuzi wake ulitokea alipokuwa akijaribu kutatua tatizo lililokabili benki wakati huo. Benki zilitaka kuhakikisha wateja wanaweza kupata pesa wakati benki zimefungwa.

Goodfellow ambaye ni mhandisi kutoka Glasgow, Scotland alikuwa ameajiriwa na benki moja na ameambia BBC kwamba wazo hilo lilimjia alipokuwa akitazama kadi iliyokuwa na data iliyoandikwa kwa lugha ya kompyuta ya ‘1’ na ‘0’, lugha ambayo hujulikana kama binary.

Alitafakari kwa kina na kugundua kwamba ni mashine pekee iliyokuwa na uwezo wa kusoma nambari hizo na kuzirejesha hadi mfumo wa nambari za kawaida.

Baadaye alitengeneza njia ya kusaidia watu kuandika nambari ya siri ya kadi (PIN) kwenye mashine kivyake mtu akitumia kibodi.

Kwa sasa, kuna shughuli zaidi ya bilioni moja ambazo hufanyika kila siku zikitumia PIN.

Haki miliki ya picha Getty

Lakini Bw Goodfellow anasema hakulipwa pesa zozote kutokana na uvumbuzi wake kwa sababu aliambiwa ubunifu wake ulizingatiwa kwenye mshahara wake.

"Hili ni jambo linalonikera sana,” anasema.

Pesa pekee alizopokea ni $15, dola moja kwa kila saini aliyoweka kwenye karatasi ya kuomba kutambuliwa kwa uvumbuzi huo katika nchi 15.

Anasema alikaa kimya kwa miaka 39 hadi pale mtu mwingine alipojitokeza na kutaka kujizolea sifa akisema ndiye aliyevumbua nambari hizo.

Mwanzoni, kulikuwa na wazo la kwa na PIN ya tarakimu tisa, sita, au nane. Mwishowe, iliafikiwa namba ambayo watu wangekumbuka kwa urahisi ni ya tarakimu nne.