Muhtasari: Habari kuu leo Jumatatu

Miongoni mwa habari kuu leo, Donald Trump anasema Uchina imeikuwa 'ikiibaka' Marekani kiuchumi, wanasayansi wanasema wamebaini virusi vya Zika vina madhara zaidi na mlanguzi wa mihadarati amesafirishwa kutoka Colombia hadi Peru.

1. Trump asema Uchina ‘imeibaka’ Marekani

Haki miliki ya picha
Image caption Trump amekuwa akiishutumu Uchina

Mgombea mkuu wa chama cha republican Donald Trump amekashifu sera za biashara za China na kuilaumu kwa kile alichokitaja kuwa "kuibaka" Marekani.

Kwenye mkutano wa kampeni katika jimbo la Indiana Trump anasema kuwa China inafanya wizi mkubwa zaidi katika historia ya dunia na hilo halitaruhusiwa kuendelea.

Trump mara kwa mara ameikashifu China kwa kukarabati sarafu yake ili kufanya mauzo yake kuwa yenye ushindani zaidi na wenye athari kubwa kwa uchumi wa marekani.

2. Wanasayansi wasema Zika ni hatari zaidi

Haki miliki ya picha
Image caption Virusi vya Zika husababisha watoto kuzaliwa na vichwa vidogo

Wanasayansi nchini Brazil wanasema kuwa virusi vya Zika huenda vikawa hatari zaidi kuliko ilivyodhaniwa awali.

Wataalamu wameiambia BBC kuwa virusi hivyo vinavyosambazwa na mbu huenda vinahusishwa na uharibifu mkubwa ambao humkumba mwanamke mmoja kati ya watano wanaoambukizwa virusi hivyo. Kawaida huaminika kusababisha hali ambapo mtoto anayezaliwa huwa na kichwa kidogo.

Akina mama walioathirika na virusi hivyo nchini Brazil wamejifungua zaidi ya watoto 1200 walio na hali kama hiyo.

3. Kerry ajaribu kuzima vita Syria

Haki miliki ya picha AP
Image caption Vita zimekuwa vikiendelea katika mji wa Aleppo

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni nchini Marekani John Kerry anasema kuwa atatafuta ushirikiano wa Urusi katika jitihada za kusitisha ukatili nchini Syria. Akizungumza alipowasili mjini Geneva wakati wa kuanza kwa jitihada za kidiplomasia za kumaliza ghasia katika mji wa Aleppo, Kerry anasema kuwa huu ni wakati ulio hatari.

Alisema anatarajia serikali ya Syria itaisikiliza urusi. Wiki moja ya mashambulizi makubwa imesababisha vifo vya zaidi ya watu 200 mjini Aleppo.

4. CIA yasema al-Qaeda wamedhoofishwa sana

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Osama aliuawa 2 Mei, 2011

Mkurugenzi mkuu wa shirika la ujasusi la marekani CIA John Brennan anasema kwa Marekani imeangamiza sehemu kubwa ya mtandao wa Al Qaeda miaka mitano tangu kiongozi wake Osama Bin Laden auawe na vikosi maalum nchini Pakistan.

Bw Brennan alisema kuwa Bin Laden alikuwa mwenye ushawishi mkubwa na ilikuwa muhimu kumuondoa mtu ambaye alihusika na kupanga na mashambulizi ya Sepetemba 11 katika miji ya New York na Washington. Mkuu huyo wa CIA pia anasema kuwa ikuwa mkuu wa kundi la Islamic State, Abu Bakr Al-Baghdadi, atauawa itakuwa na athari kubwa kwa kundi hilo.

5. Mlanguzi wa mihadarati apelekwa Peru

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ulanguzi wa mihadarati ni tatizo kubwa Peru

Colombia imemsafirisha mtu anayedaiwa kuwa mlanguzi wa madawa ya kulevya kwenda nchini peru ambaye anatajwa kuwa mtu anayetafutwa zaidi nchini humo.

Gerson Galvez alikamatwa na polisi wa Colombia siku ya Jumamosi eneo la Medellin.

Maafisa nchini Colombia walisema kuwa alisafirishwa kwenda Peru ndani ya saa 24 kwa sababu hakuwa na cheti cha kuishi nchini humo.

Galvez analaumiwa kwa kuongzoa genge moja la walanguzi wa dawa ya Cocain ambalo limehusishwa na mauaji katika bandari ya Callao nchini Peru.

6. Polisi wavamia makao ya waandishi Cairo

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanahabari wawili wanadaiwa kukamatwa

Waandishi wa habari nchini Misri wanasema kuwa polisi wamevamia makao ya chama chao kati kati mwa mji wa Cairo ambapo waliwakamata waandishi wawili wa habari wanaoikosoa serikali.

Wizara ya mambo ya ndani nchini Misri ilikana madai ya kuvamia makao ya chama hicho lakini ikakiri kuwa waandishi wawili walikamatwa.

Ripoti zinasema kuwa wawili hao walikamatwa kwa kuchochea maandamano.

7. Valls kusimamia kandarasi ya manowari

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kandarasi hiyo ni ya thamani ya dola billioni 39

Waziri mkuu wa Ufaransa Manuel Valls amesema kuwa atasimamia mwenyewe kandarasi kubwa iliyoshindwa na kampuni ya Ufaransa ya DCNS ya kujenda manowari ya jeshi la wanamaji wa Australia.

Bw Valls alikuwa akiongea kwenye mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari mjini Canberra nchini Australia na mwenzake waziri mkuu Malcolm Turnbull.

Wiki iliyopita DCNS iliwabiku washindani kutoka Japan na Ujerumani na kushinda kandarasi hiyo ya gharama ya dola billioni 39 ya kujenga manowari 12 kwa Australia.

Kampuni hiyo inasema kuwa chombo hicho chenye uzito wa tani 4500 ndicho hatari zaidi kuwai kujengwa.

8. Wanajeshi wa Uingereza wawasili Somalia

Haki miliki ya picha PA
Image caption Wanajeshi hao watasaidia wanajeshi wa AU

Kikosi kidogo cha jeshi la Uingereza kimewasili nchini Somalia kusaidia wanajeshi wa muungano wa Afrika walioko huko.

Karibu wanajeshi 10 wa uingereza watafutiwa na kikosi kingine cha wanajeshi 70.

Watasaidia kutoa huduma za matibabu, usafiri na za kiufundi.

Waziri wa ulinzi wa Uingereza Michael Fallon anasema kuwa kikosi hicho kitasaidia kuleta udhabiti na kukabiliana na tisho kutoka kwa wanamgambo nchini Somalia.