Urusi :Mkataba wa amani kuongezwa siku Aleppo

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Syria Aleppo

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kuwa mkataba wa usitishaji mapigano utaongezewa muda wa siku tatu katika jiji la Aleppo na maeneo ya Kaskazini katika mkoa wa Latakia.

Karibu raia 300 wamefariki chini ya muda wa majuma mawili kutokana na makabiliano makali ya silaha.

Utulivu umetajwa kurejea katikati mwa Aleppo. Hata hivyo makabiliano makali yangali yanaendelea Kusini ambapo wanajeshi wa Syria na waasi wa Kiislamu kukiwemo kundi la Nusra Front wamekuwa wakipigana.

Mapatano ya amani yalikuwa sehemu moja ya juhudi za kujenga msingi wa kusitisha mapigano ulioanza Februari mwaka huu.

Katika maeneo mengine ya Syria Kaskazini, kungali kuna hali ya sintofahamu juu ya mashambulizi ya ndege yaliyofanywa Alhamisi kwenye kambi za watu waliotoroka makwao. Urusi na Serikali ya Syria wamekanusha kuhusika.