Waandishi wa BBC watimuliwa Korea Kaskazini

Wingfield-Hayes
Image caption Wingfield-Hayes aliangazia maisha katika mji wa Pyongyang

Waandishi wa habari wa BBC wanazuiliwa nchini Korea Kaskazini na mwanahabari Rupert Wingfield-Hayes anatimuliwa kutoka nchi hiyo kutokana na taarifa zake.

Mwanahabari huyo, produsa Maria Byrne na mpiga picha Matthew Goddard walisimamishwa na maafisa wa serikali Ijumaa walipokuwa wakijiandaa kuondoka Korea Kaskazini.

Walihojiwa kwa saa nane na maafisa wa Korea Kaskazini na kisha wakatakiwa kutia saini taarifa.

Wote walizuiliwa wikendi yote lakini sasa wamepelekwa katika uwanja wa ndege.

Kundi hilo la BBC lilikuwa Korea Kaskazini kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa chama tawala cha Workers Party Congress, likiandamana na ujumbe wa washindi wa tuzo ya Nobel waliokuwa wakifanya utafiti.

Utawala wa Korea Kaskazini haukufurahishwa na taarifa zao zilizoangazia hali ya maisha katika mji mkuu Pyongyang.

Wingfield-Hayes alizuiwa kuabiri ndege Ijumaa na akazuiliwa.