Washtakiwa 21 wafungwa jela maisha Burundi

Burundi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maandamano yalianza Burundi Aprili mwaka jana

Mahakama ya rufaa nchini Burundi imewahukumu washtakiwa 21 vifungo vya maisha jela baada ya kuwapata na hatia ya kushiriki jaribio la mapinduzi mwaka jana.

Washtakiwa hao ni kati ya 28 waliokuwa wameshtakiwa kuhusiana na jaribio hilo la Mei mwaka jana ambalo halikufaulu.

Miongoni mwao ni watano ambao walikuwa wamepatikana bila hatia na mahakama ya kwanza.

Mahakama hiyo ya rufaa imeagiza wakamatwe.

Upande wa mashtaka ulikata rufaa dhidi ya hukumu iliyotolewa na mahakama ya chini ukisema hukumu hiyo haikuwa kali vya kutosha.

Wale waliopatikana na hatia pia wametakiwa kulipa zaidi ya $3.5m (£2.4m) kama fidia kutokana na vifo na uharibifu wa mali uliotokea wakati wa jaribio hilo la kupindua serikali.

Baadhi ya majenerali kwenye jeshi na baadi ya maafisa wakuu katika idara ya polisi walijaribu kumpindua Rais Pierre Nkurunziza baada yake kuamua kuwania urais kwa muhula wa tatu.

Uamuzi wa leo unatazamwa kama ushindi wa serikali ambayo imekuwa ikijaribu kujenga uhusiano wa moja kwa moja baina ya jaribio hilo la mapinduzi na maandamano ya kupinga hatua ya Rais Nkurunziza kuwania kwa muhula wa tatu.

Maandamano hayo yalianza wiki mbili kabla ya mapinduzi.