Katumbi atarajiwa kufika mahakamani DRC

Haki miliki ya picha
Image caption Moise Katumbi ametangaza rasmi nia ya kugombea urais DRC
Mwanamume anayetarajia kuwa mgombea mkuu wa upinzani kwa urais katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, anatarajiwa kufika mbele ya mahakama leo kujibu mashtaka yanayaomkabili ya kuwaajiri mamluki kutoka mataifa ya nje.

Mawakili wa Moise Katumbi wanasema Gavana huyo wa zamani wa jimbo lililo na utajiri wa madini - Katanga, alikabidhiwa barua ya kufika mahakamani mwishoni mwa juma na anatakiwa kufika mbele ya mwendesha mashtaka nchini humo siku ya Jumatatu.

Nyumba yake ilisakwa na walinzi wa serikali siku ya Jumamosi.

Katumbi amekana mashtaka na ameishutumu serikali kwa kutumia njia za kumchafulia jina.

Ubalozi wa Marekani mjini Kinshasa pia umetilia shaka tuhuma hizo.

Rais Joseph Kabila ambaye yupo madarakani tangu mwaka 2001 bado hajabainisha iwapo atajiuzulu mwaka huu kama inavyo takiwa kwenye katiba ya nchi.