Katumbi ahojiwa na waendesha mashtaka DRC

Katumbi Haki miliki ya picha
Image caption Katumbi amekanusha madai ya waziri wa haki

Mwanasiasa wa upinzani aliyetangaza atawania urais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Moise Katumbi amehojiwa na maafisa wa mashtaka mjini Lubumbashi.

Hii ni baada ya serikali kumtuhumu kwa kuwaajiri mamluki kutoka nje.

Shirika la habari la Reuters linasema polisi walirusha mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya mamia ya wafuasi wa Bw Katumbi waliomfuata hati kwenye afisi ya mwendesha mashtaka mkuu.

Alipokuwa akihojiwa, wafuasi hao walikuwa wakiimba “rais!”.

Baadhi waliingia katika majengo hayo na mmoja wa walioshuhudia ameambia Reuters kwamba wanne walikamatwa.

Bw Katumbi ametanusha madai yaliyotolewa na waziri wa haki wiki iliyopita kwamba aliwaajiri mamluki, wakiwemo wanajeshi kutoka Marekani.

Wafuasi wake wanasema madai hayo yanalenga kuvuruga juhudi zake za kutaka kumrithi Rais Joseph Kabila.

Serikali imekanusha madai kwamba Katumbi anaandamwa kwa sababu za kisiasa.

Uchaguzi mkuu unafaa kufanyika baadaye mwaka huu.