Man United kuchuana na West Ham

Image caption Manchester United

Manchester United inatarajiwa kuimarisha mikakati yake ya kujikatia tikiti ya kushiriki katika fainali za kombe la klabu bingwa barani Ulaya msimu ujao, baadaye leo usiku wakati watasafiri ugenini kuchuana na West Ham.

Manchester City ilitoka sare na Arsenal mwishoni mwa juma lililopita na hivyo kumaanisha ikiwa Manchester United itaipiku West Ham, basi itakuwa imejizolea alama zaidi kuliko mahasimu wao Manchester City, na kuwa katika nafasi ya nne.

Hata hivyo Manchester United ni sharti ishinde mechi yao ya mwishi dhidi ya Bournemouth siku ya Jumapili, ili kujihakikishia nafasi hiyo ya nne.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Louis Van Gaal

Lakini kocha wa West Ham, Slaven Bilic amesema vijana wake ni sharti wawe makini katika mechi yao ya mwisho katika uwanja wao wa nyumbani wa Upton Park msimu huu.

West Ham ambayo haina nafasi katika nne bora inapania kujikatia tikiti ya kushiriki katika kinyang'anyiro cha kuwania kombe la Europa msimu ujao.

Mechi hiyo pia itakuwa ya mwisho ya West Ham katika uwanja huo, kwa kuwa wanahamia uwanja mpya msimu ujao.

West Ham imewahi kucheza mechi 2,398 katika uwanja huo na Billic amesema kuwa mechi hio ina umuhimu mkubwa katika historia ya klabu hiyo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption West Ham

West Ham kwa sasa iko katika nafasi ya saba baada ya kunyukwa magoli 4-1 na Swansea siku ya Jumamosi, alama moja chini ya Southampton ambayo ingali na mechi moja zaidi.

Timu zitakazomaliza katika nafasi ya tano na sita zitafuzu moja kwa moja kwa kombe la Europa.