Muhtasari: Habari kuu leo Jumanne

Miongoni mwa habari nyingine kuu leo, Rodrigo Duterte anakaribia kushinda Ufilipino, meya wa Alberta, Canada amesema uokoaji wa watu ulikuwa muujiza na wanasayansi wanasema mimea mingi imo hatarini ya kuangamia.

1. Mwanasiasa mwenye msimamo mkali aongoza Ufilipino

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Duterte alipiga kura yake mjini Davao, kusini mwa Ufilipino

Ulingo wa kisiasa nchini Ufilipino umeshuhudia mabadiliko makubwa baada ya dalili za ushindi wa Rodrigo Duterte katika uchaguzi wa urais.

Huku ikiwa karibu kura zote zimehesabiwa Bw Duterte anaongoza kwa kura nyingi.

Aliongoza kampeni iliyojawa matusi na utata mkubwa lakini rekodi yake kama meya wa mji wa kusini mwa Ufilipino ambao kwa wakati moja ulishuhudia viwango vya juu vya uhalifu, huenda iliwashawishi wapiga kura kwamba ataweza kukabiliana na uhalifu pamoja na ufisadi uliopo nchini humo.

2. Mkuu wa Alberta asema uokoaji ulikuwa muujiza

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Moto huo ulisababisha uharibifu mkubwa

Mkuu wa jimbo la Alberta nchini Canada ameutaja kama muujiza operesheni kubwa ya kuwaondoa watu katika mji wa Fort McMurray uliogubikwa katika moto mkubwa unaoteketeza misitu ya taifa hilo.

Rachel Notley alikuwa akizungumza baada ya kuuzuru mji huo wenye utajiri wa mafuta ambao zaidi ya wakaazi 80,000 walihamishwa.

3. Serikali kuu Marekani yaishtaki North Carolina

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Sheria mpya North Carolina inatambua jinsia iliyo kwenye vyeti vya kuzaliwa

Idara ya sheria nchini Marekani imeifungulia mashtaka serikali ya jimbo la North Carolina pamoja na gavana wake ili kuzuia utekelezwaji wa sheria mpya kuhusu jinsia.

Sheria hiyo inawalazimisha watu waliobadili jinsia kutumia vyoo vinavyokwenda sambamba na jinsia waliyotambuliwa nayo wakati wa kuzaliwa.

Mkuu wa sheria, Loretta Lynch, amesema anatafakari kusitisha msaada unaotolewa na serikali kuu kufadhili taasisi za serikali ya jimbo la North Carolina.

4. Uiongereza yaonywa kuhusu kujitoa EU

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bw Obama ni mmoja wa viongozi mashuhuri wasiotaka Uingereza ijitoe EU

Uingereza imeonywa kwamba hadhi yake kimataifa itatokomea ikiwa itaamua kujiondoa katika Muungano wa Ulaya. Katika barua iliyochapishwa katika gazeti la The Times, mawaziri wa ulinzi kumi na watatu wa zamani nchini Marekani pamoja na wakuu wa sera za kigeni wamesema kuwa Uingereza na ulaya itapoteza ushawishi katika sera za kigeni na ulinzi pamoja na biashara ya kimataifa ikiwa Uingereza itajiondoa.

5. Wanasayansi watahadharisha kuhusu chanjo

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Angola ni moja ya nchi zilizotatizwa sana na homa ya manjano

Wanasayansi nchini Marekani wameonya kuwa ukosefu wa chanjo dhidi ya homa ya manjano huenda ukasababisha tatizo kubwa la kiafya na usalama.

Wametoa wito kwa shirika la Afya duniani WHO kuchukua hatua za dharura kurekebisha hali hiyo.

Maprofesa wawili kutoka chuo kikuu cha Georgetown wanasema ugonjwa huo ambao umezuka nchini Angola na kuwaambukiza zaidi ya watu 2,000 huenda ukaenea katika mataifa mengine.

6. Wataalamu wagundua mimea 2,000 mipya

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Asilimia 20 ya mimea duniani imo hatarini

Na ripoti mpya kuhusu mimea duniani inasema kuwa zaidi ya aina mpya ya mimea 2,000 iligunduliwa mwaka uliopita pekee.

Lakini watafiti kutoka taasisi ya Royal Botanic Gardens mjini London, wameonya asilimia 20 ya mimea yote duniani inakabiliwa na hatari ya kuangamia kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, uharibifu wa mazingira na ugonjwa.