Trump: Meya Mwislamu anakaribishwa Marekani

Khan
Image caption Khan ndiye Mwislamu wa kwanza kuwa Meya wa London

Mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump amesema meya mpya wa jiji la London ambaye ni Mwislamu hangezuiwa kuzuru Marekani iwapo pendekezo lake kwamba Waislamu wazuiwe kwa muda kuingia Marekani lingetekelezwa.

Kwa sababu ya imani yake, meya huyo mpya Sadiq Khan amesema ana shaka kuhusu iwapo ataruhusiwa kuzuru Marekani iwapo Bw Trump atachaguliwa kuwa rais.

Bw Trump alipendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani baada ya watu 130 kuuawa kwenye mashambulio ya kigaidi mjini Paris Novemba mwaka jana na baadaye shambulio la San Bernardino, California lililoua watu 14.

“Kutakuwa na hali za kipekee,” mfanyabisahara huyo tajiri kutoka New York amesema.

Pendekezo la Bw Trump lilishutumiwa sana Marekani nan je ya nchi hiyo lakini mwanasiasa huyo amezidi kutetea pendekezo hilo akisema hatua hiyo inahitajika kuhakikisha usalama wa Marekani.

Bw Trump amesema ana furaha kwamba Bw Khan ataongoza jiji la London.

“Akifanya kazi nzuri na kwa kweli akifanya kazi nzuri sana, hilo litakuwa jambo njema sana,” ameongeza.

Bw Khan, wa chama cha Labour, ambaye ni mwana wa wahamiaji kutoka Pakistan, ndiye meya wa kwanza wa London kuwa Mwislamu.

Image caption Bw Khan hupenda sana kucheza kandanda

Alishinda mpinzani wake wa chama cha Conservative Zac Goldsmith kwa kupata kura 1,310,143 dhidi ya 994,614.

"Ningependa kwenda Marekani na kukutana na mameya wa miji ya Marekani,” Bw Khan aliambia gazeti la Time.

"Iwapo Donald Trump atachaguliwa kuwa rais, nitazuiwa kufanya hivyo kwa sababu ya imani yangu.”

Aliongeza kwamba ana imani kwamba mtazamo wa Donald Trump kuhusu siasa hautafanikiwa nchini Marekani.