Serikali ya Nigeria yamjibu Cameron

Nigeria imeshangazwa na kusikitishwa na kauli iliyotolewa na waziri mkuu wa Uingereza kwamba nchi hiyo inaongoza kwa rushwa.

David Cameron aliitaja Nigeria na Afghanistan kuwa ni nchi mbili duniani zinazoongoza kwa rushwa na ufisadi.

Ingawa kauli hiyo hakuitoa rasmi kwa vyombo vya habari, lakini Bwana Cameron ameonekana katika kamera akiwa ndani ya kasri ya Buckingham akimwambia malkia Elizabeth kwamba viongozi wa baadhi ya nchi ambazo zinaongoza kwa ufisadi duniani watahudhuria mkutano dhidi ya ufisadi unaotarajiwa kuanza hapo kesho chini ya uwenyeji wa David Cameron.

Garba Shehu msemaji wa Rais Muhammadu Buhari anasema wameshangazwa na kuhuzunishwa na kauli hiyo kwa sababu imeshindwa kuzingatia kwazi kubwa inayofanywa na rais Buhari kuondoa rushwa serikali.

'' Tunaamini kwamba waziri mkuu alikua akiangalia picha ya zamani ya Nigeria, ambayo tayari imeondolewa, dunia nzima inaangalia mapambano yanayofanyika dhidi ya rushwa, na tunaamini ni kutokana na mafanikio hayo ndio Rais Buhari amealikwa sio tu kama mgeni bali miongoni mwa watakaotoa mada." alisema.

Agenda kuu iliyomwingiza madarakani Rais Buhari ni ile ya kutokomeza rushwa na kupambana na kundi la Boko Haram na kuhakikisha kuwa wanafunzi wa kike waliotekwa na kundi hilo, wanapatikana. Hata hivyo, kadri siku zinavyokwenda, ndivyo ugumu wa kupatikana kwa wasichana hao unavyodhihirika na matumaini kutoweka.