Rwanda mwenyeji wa Kongamano la uchumi

Haki miliki ya picha

Kongamano la 26 la uchumi duniani linaanza leo mjini Kigali Rwanda.

Hii ni mara ya kwanza kongamano hilo kuandaliwa Rwanda na mara yake ya pili kufanyika afrika mashariki.

Kongamano hilo litakalowaleta pamoja marais wa mataifa ya Afrika wakiongozwa na mwenyeji, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, litaangazia masuala ya kiuchumi barani afrika.

Mawaziri wa masuala ya uchumi kutoka mataifa tofuati, wawakilishi wa serikali, wafanyibiashara na wawekezaji maarufu Afrika watashiriki katika mazungumzo hayo.

Kulingana na msemaji wa kongamano hilo, Oliver Cann, mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na sekta za kibinafsi ili kimarisha uchumi wa Afrika.

Suala kuu litakalojadiliwa katika kongamano hilo ni matumizi ya teknolojia kuimarisha biashara Afrika na kuyaunganisha mataifa ya Afrika ili kustawisha biashara.

Kongamano hilo linatarajiwa kutoka mapendekezo juu ya athari za teknolojia kwa ajira na uzalishaji.

Mataifa ya Afrika mashariki yametajwa kuwa mojawapo wa mataifa ya Afrika yenye uwezo mkubwa wa ukuaji na yamekuwa yakilengwa na wawekezaji.

Kongamano hilo la kimataifa litakalowaleta pamoja washiriki 1,500 linatarajiwa kukamilika siku ya Ijumaa, Mei 13.