Marekani yagoma kuiomba radhi Hiroshima

Haki miliki ya picha AP

Marekani imesema Rais Barack Obama hataomba radhi kwa shambulio la bomu la Atomu lililofanywa na nchi yake, Hiroshima Japan.

Ikulu ya Marekani imeweka bayana hayo, pindi Rais Obama atakapofanya ziara ya kihistoria katika mji huo mwishoni mwa mwezi huu.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais wa Marekani aliye madarakani kutembelea eneo hilo tangu liliposhambuliwa mnamo mwezi Agosti mwaka 1945, hivyo kusababisha vifo vya watu zaidi ya laki moja na nusu.

Shambulio hilo lilikuwa la kwanza la kikatili la matumizi ya silaha ya nuklia na lilirudiwa siku tatu baadae katika mji wa Nagasaki.

Inafahamika kwamba, mashambulio hayo ndio yaliyoshinikiza vikosi vya Japan kusalimu amri hivyo kufikia mwisho wa vita vya pili duniani.