Muhtasari: Habari kuu leo Jumatano

Miongoni mwa habari kuu leo, kiongozi wa Kiislamu Bangladesh amenyongwa na mwanamke wa miaka 72 akajifungua mtoto India.

1. Dilma Rousseff aomba usaidizi mahakamani

Haki miliki ya picha Getty

Rais wa Brazil, Dilma Rousseff, ameitaka mahakama ya juu zaidi nchini humo kuzuia vikao vya kumng'oa madarakani katika jaribio lake la mwisho kukomesha mchakato huo kabla ya kupigwa kwa kura muhimu katika bunge la Senati. Mawakili wake wamekata rufaa ya mwisho katika mahakama hiyo wakidai kuna upendeleo pamoja na udanganyifu katika mchakato huo.

2. Sanders amshinda Clinton mchujo wa West Virginia

Haki miliki ya picha Reuters

Vyombo vya habari nchini Marekani vimebashiri kuwa mgombea wa tiketi ya chama cha Democratic kwa ajili ya uchaguzi wa urais Bernie Sanders ameshinda kura ya mchujo katika jimbo la West Virginia.

Hata hivyo mpinzani wake Hillary Clinton bado anashikilia uongozi kwa jumla katika kinyang'anyiro cha kugombea tiketi ya chama hicho.

3. Kiongozi wa Kiislamu anyongwa Bangladesh

Haki miliki ya picha AFP

Bangladesh imetoa hukumu ya kifo na kumnyonga kiongozi wa chama kikuu cha Waislamu wenye itikadi kali nchini humo kwa uhalifu uliotokea wakati wa vita vya uhuru kutoka Pakistan mwaka 1971.

Motiur Rahman Nizami, kiongozi wa chama cha Jamaat-e-Islami alipatikana na hatia ya mauaji ya kimbari na ubakaji wakati wa vita hivyo.

4. Wapelelezi Marekani wamhoji aliyemtibu Prince

Haki miliki ya picha Getty

Wapelelezi katika jimbo la Minnesota nchini Marekani wamemhoji daktari mmoja aliyemtibu nyota wa muziki wa Pop Prince majuma mawili kabla ya kifo chake.

Taarifa ya polisi imefichua kwamba Dkt Michael Schulenberg alimpa dawa mwimbaji huyo aliyekuwa na umri wa miaka 57 siku moja kabla ya kifo chake mwezi uliopita.

5. Polisi wakabiliana na waandamanaji Ufaransa

Haki miliki ya picha AFP

Polisi nchini Ufaransa wamekabiliana na waandamanaji walioingia barabarani baada ya serikali kulazimisha utekelezaji wa mageuzi katika sheria za wafanyikazi.

Awali baraza la mawaziri lilikubali kutumia madaraka ambayo ni nadra sana kutumiwa kuidhinisha mageuzi hayo bila ya ushauri wa bunge.

6. Mwanamke wa miaka 72 ajifungua mtoto

Image caption Kaur alipokea matibabu kwa wiki mbili

Kliniki moja ya uzazi nchini India imesema kuwa mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 72 amezaa mtoto wake wa kwanza baada ya kupachikwa mimba kwa njia ya kitaalamu inayofahamika kama IVF.

Daljinder Kaur alizaa mtoto wa kiume mwezi uliopita baada ya matibabu yaliyodumu miaka miwili katika kliniki hiyo iliyopo katika jimbo la Haryana.

Mume wake ana umri wa miaka 79.