Dilma Rousseff ashtumu ''mapinduzi dhidi yake''

Haki miliki ya picha epa
Image caption Dilma Rousseff

Rais wa Brazil Dilma Rousseff ameshtumu hatua ya kumshtaki kuwa ''mapinduzi na mchezo'' akikana kutekeleza uhalifu wowote.

Alikuwa akilihutubia taifa katika runinga,ikiwa ni matamshi yake ya kwanza tangu maseneta kupiga kura usiku kucha kumsimamisha kazi na kumshtaki.

Bi Rousseff amesema kuwa serikali yake inahujumiwa.

Makamu wa rais Michel Temer atakuwa kaimu rais huku kesi ya Roussef ikiendelea.

Kesi hiyo huenda ikachukua takriban siku 180,ikimaanisha kwamba bi Roussef hatosimamia michezo ya Olimpiki itakayofanyika mjini Rio de Janeiro,ambayo inaanza mwezi Agosti tarehe 5.

Maseneta walipiga kura ya kumsimamisha kazi kwa kura 55 dhidi ya 22 baada ya kikao cha usiku kucha kufanyika kwa saa 20.

Image caption Rais Dilma Rousseff akihutubia taifa

Bi Roussef anatuhumiwa kwa kufanya udanganyifu wa kifedha ili kuficha deni la serikali yake wakati uchaguzi mkuu wa mwaka 2014 ulipokuwa ukikaribia.

Katika hotuba yake ,bi Rousseff amesema kuwa huenda alifanya makosa lakini hakutekeleza uhalifu wowote,''sikukiuka sheria za bajeti''.

Alisema:Kile kilichopo ni heshima na uhuru wa wapiga kura na katiba ya raia wa Brazil.