Kundi la Wahindi lamuombea Trump ashinde urais

Trump Haki miliki ya picha EPA
Image caption Trump anatarajiwa kuwa mgombea urais wa chama cha Republican

Kundi moja nchini India limefanya maombi kumuombea ushindi mgombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump.

Kundi hilo kwa jina Hindu Sena, linaloegemea siasa za mrengo wa kulia, linasema linamuunga mkono Trump kwa sababu “ndiye tumaini pekee kwa binadamu katika vita dhidi ya ugaidi wa Kiislamu”.

Wafuasi kadha wa kundi la Hindu Sena waliwasha moto na kufanya maombi katika bustani moja mjini Delhi siku ya Jumatano.

Kadhalika walikuwa na bango la kutangaza uungwaji mkono wao kwa Bw Trump.

Walikuwa wamezungukwa na sanamu za miungu wa Kihindi.

"Ni Donald Trump pekee anayeweza kuokoa binadamu," Vishnu Gupta, mwanzilishi wa kundi hilo aliambia shirika la habari la Associated Press.

Haki miliki ya picha EPA

Aliambia gazeti la The Indian Express kwamba kundi hilo limepanga hafla kadha za kudhihirisha uungaji mkono wao wa dhati kwa Bw Trump.

Bw Trump amependekeza Waislamu wazuiwe kuindia Marekani, hatua iliyomfanya kushutumiwa vikali.

Wiki hii, baada ya meya wa London Sadiq Khan ambaye ni Mwislamu kusema huenda asipate fursa ya kuzuru Marekani iwapo Trump atashinda, mfanyabiashara huyo kutoka New York alijiteta kwamba baadhi ya mambo ni ya kipekee na meya huyo hawezi kuzuiwa.

Haki miliki ya picha EPA

Baadaye Bw Trump alionekana kulegeza msimamo zaidi na kusema hilo lilikuwa pendekezo tu.

Bw Trump pia ametetea kuuawa kwa familia za magaidi na kuvamiwa kwa Syria ili kuangamiza kundi linalojiita Islamic State na kutwaa mafuta.