Muhtasari: Habari kuu leo Ijumaa

Miongoni mwa habari kuu leo, kaimu kiongozi wa Brazil Michel Temer amehimiza umoja nchini humo na kiongozi wa Hezbollah ameuawa na Israel nchini Syria.

1. Kiongozi mpya Brazil ahimiza umoja

Haki miliki ya picha AP
Image caption Temer amehimiza kuwemo umoja wa kitaifa

Kaimu rais mpya wa Brazil, Michel Temer, ametoa wito kwa raia wa taifa hilo kuunga mkono serikali yake na kufanya kazi kwa pamoja kujenga upya sifa ya serikali baada ya mgogoro wa kisiasa ulioikumba nchi hiyo.

Bw Temer amesema michezo ya Olimpiki mjini Rio mwezi Agosti, itatoa fursa kwa Brazil kuuonyesha ulimwengu hali halisi ya kiuchumi na kisiasa nchini humo.

Alikuwa akizungumza katika hotuba yake ya kwanza kabisa tangu kuchukua hatamu kutoka kwa Dilma Rousseff aliyeondolewa madarakani kwa muda akisubiri mchakato wa kumtimua ukamilike.

2. Wanajeshi wa Syria wazuia msafara wa msaada

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Urusi imekuwa ikisaidia wanajeshi wa Syria

Vikosi vya serikali nchini Syria vimezuia msafara wa magari ya kutoa msaada wa kimataifa kuelekea katika kitongoji cha Daraya kilichozingirwa katika mji wa Damascus.

Msaada huo ungekuwa wa kwanza kutolewa kwa Daraya katika kipindi cha miaka mitatu unusu.

Umoja wa Mataifa umesema jeshi lilizuia msafara huo wa magari kwa sababu yalikuwa yamebeba maziwa ya watoto.

3. Kiongozi wa Hezbollah auawa Syria

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Badreddine anadaiwa kuwa wa pili kwa ukuu Hezbollah

Kundi la wanamgambo wa, Hezbollah, limesema kuwa mmoja wa makamanda wake wa ngazi ya juu, Mustafa Badreddine, ameuwawa.

Ripoti za vyombo vya habari zinasema kuwa aliuwawa katika shambulizi la anga lililotekelezwa na Israeli ndani ya Syria.

Anasemekana kuwa afisa wa pili wa ngazi ya juu katika Hezbollah.

4. Kamanda wa Marekani aliyezuiliwa Iran afutwa

Haki miliki ya picha IRIB NEWS
Image caption Wanajeshi hao wa Marekani walipotea njia baharini

Jeshi la wanamaji la Marekani limesema kuwa limemfuta kamanda wa mabaharia kumi wa Marekani waliokamatwa na kuzuiliwa kwa muda na Iran mwezi Januari.

Mabaharia hao walikuwa wamepotea baharini kabla ya kukamamatwa na kuhojiwa nchini Iran kwa kipindi cha saa kumi na tano.

5. Bunge la Uingereza lakosoa EU

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bunge la Uingereza lakosoa EU kuhusu wahamiaji

Kamati ya bunge la Uingereza imekosoa operesheni ya Muungano wa Ulaya kukabiliana na biashara ya kusafirisha watu kimagendo katika bahari ya Mediterranean.

Kamati hiyo imesema kuwa meli za muungano huo zimewaokoa maelfu ya wahamiaji lakini zimeshindwa kuvunja mtandao wa kihalifu wa usafirishaji wa binadamu.