Kongamano la teknohama lasaka ubunifu TZ

Image caption Kongamano la teknohama Tanzania

Teknohama na mawasiliano ni tasnia zinazokua kwa kasi sana Afrika Mashariki.

Nchi ya Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo zimewekeza takriban zaidi ya dola milioni 180 katika kupanua mkongo wa taifa.

Leo Kongamano la Sahara Spark linaloendelea jijini Dar es salaam,likiwa na maadhumuni ya kukuza ubunifu wa wanateknohama nchini hasa wanawake wanaoonekana kutoshiriki katika tasnia hiyo.

Kongamano la Sahara Sparks ni mkusanyiko wa vijana ambao ni wabunifu, wajasiriamali,serikali na wafadhili likiwa na lengo la kuona namna gani ubunifu na ujasiriamali vinaweza kutatua changamoto zinazokabili umma.

Caroline Ekyarisiima ni mwanzilishi wa taasisi ya 'apps and girls'.

Taasisi yake inawafundisha wasichana wa umri wa miaka 10 had 18 jinsi ya kutumia teknohama kutengeneza miradi ya kusaidia jamii zao.

Caroline ambaye alikuwa mwalimu wa sekondari anasema alianza na wasichana wachache lakini sasa anaona muamko wa wasichana wakitamani kujifunza zaidi.

Image caption Baadhi ya ubunifu katika kongamano hilo

Caroline pia anasema ili kuendeleza sekta hiyo zaidi, serikali haina budi kupitia tena mfumo wa elimu na kuongeza masomo ya teknohama mapema kwa watoto.

Winnie ni mmoja wa wanafunzi waliopata mafunzo katika taasisi hio, akiwa na miaka 16 tu. Ametengeneza tovuti ya kukuza uelewa wa ugonjwa wa fistula pamoja na tovuti inayowawezesha wanafunzi kutoamalalamiko ya unyanyasaji na udhalalishaji wakiwa katika usafiri wa daladala.

Ubunifu wake umemshindia nafasi kwenye shule maarufu ya Africa Leadership Academy Afrika ya Kusini.