Mirungi marufuku katikati ya wiki Aden

Mirungi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maafisa wa jeshi walizuia wafanyabiashara kuingia na mirungi

Maafisa katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Yemen, mji wa Aden, wamepiga marufuku uuzaji wa mirungi katikati ya wiki.

Masoko ya uuzaji wa mirungi yalisalia kwua wazi Jumatatu na wanajeshi wanaounga mkono serikali walizuia magari yaliyobeba bidhaa hiyo kuingia mjini.

Marufuku hiyo ilitolewa baada ya baadhi ya wakazi kulalamika kuhusu “usalama, masuala ya kijamii na afya”.

Utafiti wa awali umeonesha kuwa karibu 90% ya wanaume Yemen na 50% ya wanawake hutafuna mirungi, ambayo pia hujulikana kama miraa.

Baadhi hutazama hilo kama kosa kubwa katika jamii.

Vizuizi vimewekwa katika barabara za kuingia mji wa Aden kuzuia watu kuingia na mirungi, shirika la AFP linasema.

Uuzaji wa miraa utaruhusiwa Alhamisi na Ijumaa pekee, ambazo huwa ndizo siku za wikendi Yemen.

Haki miliki ya picha BBC World Service

Mmoja wa wachuuzi Abdu Hazaa aliambia shirika la habari la Associated Press kwamba baadhi ya shehena yake ya mirungi iliteketezwa, lakini alifanikiwa kununua nyingine.

Mirungi ni marufuku Marekani na katika Muungano wa Ulaya na Khat, na Shirika la Afya Duniani limeiorodhesha kama dawa ya kulevywa ambayo inaweza kusababisha “uraibu na utegemezi wa kiwango cha kadiri”.

Miraa inaweza pia kuathiri mdomo na kuharibu meno na kuna wasiwasi huenda ikawa inachangia saratani ya midomo.