Muhtasari: Habari kuu leo Jumanne

Miongoni mwa habari nyingine kuu leo, ulinzi mkali umewekwa Hong Kong huku afisa mkuu wa Uchina akijiandaa kuzuru na mwanamume aliyepandikizwa uume Marekani ameeleza furaha yake.

1. Ulinzi mkali wawekwa Hong Kong

Haki miliki ya picha BBC Chinese

Ulinzi umeimarishwa nchini Hong Kong, huku Zhang Dejiang afisa wa ngazi ya juu zaidi kutoka Uchina akizuru eneo hilo, tangu maandamano ya kidemokrasia ya mwaka wa 2014.

Polisi wapatano 6,000 wametumwa katika eneo hilo na mawe yaliyoko barabarani yameunganishwa kwa nta ili kuzuia waandamanaji kuyang’oa na kuyatumia kama silaha.

Aidha utawala wa eneo hilo umejenga ua wenye urefu wa mita mbili kuzuia umati wa watu.

Makundi kadhaa ya wanaharakati wa kijamii yamesema kuwa yanapanga kuandamana wakati wa ziara hiyo, huku baadhi yao wakipanga kuandamana hadi jengo kuu la serikali kati kati mwa mji, ambako hafla maalum ya kumlaki Bw Zhang itafanyika.

2. Marekani kuipa silaha serikali ya Libya

Haki miliki ya picha Reuters

Mataifa 25, ikiwemo Marekani yameafikiana kuipa serikali ya Libya silaha ili kuzuia wapiganaji wa Islamic State kudhibiti taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika.

Muungano huo wa kimataifa umesema utalegeza vikwazo vya ununuzi wa silaha vya Umoja wa Mataifa kuhusu Libya na kutoa misaada ya silaha na zana nyingine za kivita kwa wanajeshi watiifu kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyo na makao yake mjini Tripoli.

Waziri mkuu wa Libya, Fayez al-Sarraj, amesema kundi hilo la Islamic State ni tishio kubwa kwa usalama wa taifa hilo na kanda hiyo, na kuwa msaada wa kigeni unahitajika zaidi, ikiwa utawala wa nchi hiyo unadhamira ya kufanikisha vita dhidi ya ugaidi.

Wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walikubaliana mkataba huo kwenye mazungumzo yaliyofanyika mjini Vienna, Austria.

3. Wanadiplomasia kufufua mazungumzo ya Syria

Haki miliki ya picha Reuters

Wakati huo huo, wanadiplomasia wanakutana mjini Viena hii leo kujaribu kufufua mazungumzo ya amani kuhusu Syria.

Mazungumzo hayo yatahusisha wanachama wa jopo maalum la kimataifa kuhusu Syria linalojumuisha mataifa ya Marekani, Urusi, Iran na mataifa ya Kiarabu.

Mazungumzo mengine kati ya makundi hasimu nchini Syria, yaliyofanyika mjini Geneva, Aprili mwaka huu yalisambaratika, wakati kundi la upinzani lilipojiondoa, kutokana na kuongezeka kwa ghasia na machafuko nchini Syria.

4. Mexico yatakiwa ipige marufuku uvuvi

Haki miliki ya picha BBC World Service

Shirika la kuhifadhi wa wanyama wa mazingira la World Wildlife Fund, limetoa wito kwa serikali ya Mexico kupiga marufuku uvuvi, katika eneo wanakopatikana aina moja ya nyangumi wanaofahamika kama vaquita porpoises.

Hii ni baada ya idadi ya nyangumi hao kupungua kwa 40% katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Wiki iliyopita, ilitangazwa kuwa ni nyangumi 60 pekee wa aina hiyo waliosalia kote duniani.

Wanyama hao ambao ni waoga, ndio wadogo zaidi katika familia ya nyangumi na wanapatikana katika ghuba ya California.

Nyangumi hao huvuliwa na kuuzwa kimagendo nchini Uchina.

5. Wafanyakazi wa mafuta kuhamishwa Canada

Haki miliki ya picha AFP

Utawala nchini Canada umeagiza zaidi ya wafanyakazi 600 wa kampuni moja ya mafuta katika mkoa wa Alberta kuhamishwa kutokana na moto mkubwa unaoendelea kuteketeza misitu katika eneo hilo.

Waziri mkuu wa mkoa huo Rachel Notley amesema watu wanaoishi karibu na kambi ya Fort McMurray wamehamishwa hadi kambi moja ya kampuni hiyo iliyoko eneo la Kaskazini, ambako maelfu ya wafanyakazi wengine wamewekwa katika hali ya tahadhari.

Ripoti kutoka maeneo hayo zinasema kuwa moshi mkubwa wa rangi ya manjano umetanda angani ukiwa umechanganyika na majivu.

6. Hali ya tahadhari yatangazwa Venezuela

Haki miliki ya picha AFP

Serikali ya Venezuela imetoa maelezo zaidi kuhusu hali ya tahadhari iliyotangazwa na rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro, huku mzozo wa kiuchumi na kisiasa ukiendelea kukumba taifa hilo.

Tahadhari hiyo itadumu kwa siku sitini na huenda muda huo ukaongezwa kwa siku nyingine sitini.

Majeshi ya nchi hiyo na kamati za mitaa zimepewa mamlaka ya kusambaza na kuuza vyakula.

Aidha utawala wa nchi hiyo unaweza kupunguza idadi ya siku ambazo wafanyakazi watakuwa wakihudumu kwa wiki katika sekta ya kibinafsi ili kuhifadhi umeme.

Maduro amesema mikakati hiyo ni muhimu ili kuzuia uchumi wa taifa hilo kusambaratika zaidi.

Upinzani kwa sasa unajaribu kumuondoa madarakani.

7. Mwanamume apandikizwa uume Marekani

Haki miliki ya picha AP

Raia mmoja wa Marekani ambaye alifanyiwa upasuaji wa kupandikiza sehemu uume, ameiambia BBC kuwa anatarajia upasuaji huo, utatoa matumaini kwa mashujaa wa vita ambao walipoteza sehemu zao nyeti.

Thomas Manning, ambaye alikuwa na umri wa miaka 64, amesema wakati bomu lilipolipuka, liliharibu miguu yake yote na haikuishia hapo.

Manning amesema alikuwa na matumaini makubwa ya kupata kiungo kipya baada ya uume wake kuondolewa wakati alipougua ugonjwa wa saratani.

Hata hivyo amesema anajuta kuwa ilikuwa lazima mtu mwingine ili dhamira na nia yake itimizwe.

Madaktari mjini Boston wametaja upasuaji huo kama wa kihistoria.